Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC ataka weledi utekelezaji wa Tasaf

F946fc6c90dd0bd94b057571fded9c27 DC ataka weledi utekelezaji wa Tasaf

Wed, 21 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Vumilia Nyamoga ametaka kuwepo kwa umakini na uadilifu ili kufikia malengo ya serikali wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).

Alisema hayo juzi wakati wa akifungua kikao kazi cha kujenga uelewa wa wadau kuhusu sehemu ya pili ya awamu ya tatu ya TASAF.

Alisema halmashauri hiyo imejizatiti kuhakikisha kuwa malengo ya mpango huo yanafikiwa sambamba na kuhakikisha wote walioainishwa na kuandikishwa kwenye mpango wananufaika.

“Ili malengo hayo yafikiwe kwa ukamilifu ushiriki wa wadau wote katika ngazi mbalimbali unahitajika sana, muundo wa sehemu ya pili ya mpango umezingatia sana changamoto ambazo zilijitokeza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza,” alisema

Alisema usimamizi na ufuatiliaji umeimarishwa katika ngazi ya mkoa , halmashauri na kata kwa kuhusisha watumishi zaidi kufuatilia shughuli za mfuko.

“Tukafanye kazi kwa uadilifu ili tufikie malengo ya serikali kupitia

kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Tasaf ya kupunguza umaskini na

kuchochea ukuaji wa uchumi ukiwemo ule wa viwanda ambavyo ni agenda

muhimu ya serikali,” alisema.

Katika hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga iliyosomwa na Mtaalamu wa utafifi wa TASAF, Tumpe Lukongo, alisema tathimini ya utekelezaji wa kipindi cha kwanza awamu ya tatu inaonesha mpango umechangia kwa kiasi kufikia azma ya serikali ya kupunguza umaskini nchini.

Alisema takwimu zinaonesha utekelezaji wa mpango kwa kipindi cha kwanza umechangia kupunguza umaskini wa mahitaji ya msingi kwa kaya kwa asilimia 10 na umaskini uliokithiri umepungua kwa asilimia 12 kwa kaya maskini sana nchini kote.

Pia utekelezaji wa mpango umewezesha kaya za walengwa kujikita katika shughuli za kukuza kipato na kujiimarisha kiuchumi ikiwemo ufugaji, uvuvi, kilimo na biashara ndogo ndogo.

Alisema baada ya kukamilika kipindi cha kwanza, serikali iliamua kuendelea na kipindi cha pili katika awamu ya tatu ili kaya zote zinazoishi katika mazingira duni zipate usaidizi wa serikali kupitia TASAF kwa kuwawezesha kufanya kazi na kupambana na umaskini.

Alisema kipindi cha pili kilianza kwa uhakiki wa walengwa wote na kuondoa kaya zote za walengwa ambazo zimepoteza sifa.

“Hapo nyuma kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu mpango kuwa na watu wasiostahili wakiwemo watu wasio maskini, viongozi, orodha ya walengwa kuwa na watu waliohama au waliofariki ambao hao wote waliitwa walengwa hewa, utekelezaji ulianza kwa kusafisha daftari la walengwa,” alisema.

Alisema katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu mradi utatekelezwa katika halmashauri 184 za Tanzania bara na wilaya zote za Zanzibar na utafikia kaya 1,450,000 zenye jumla ya watu zaidi ya milioni saba kote nchini ikiwa ni nyongeza ya kaya 350,000

“Mkazo mkubwa utawekwa katika kuwezesha kaya zitakazoandikishwa kwenye mpango kufanya kazi ili kuongeza kipato, huduma za jamii zinaongezwa na kuboreshwa ili kutoa huduma na kuendeleza raslimali watoto hususan katika upatkanaji wa elimu na afya.

Kwa upande wake Katibu Tawala wilaya ya Chamwino, Juliana Kilasara aliwata watekelezaji wa mpango huo kila mmoja asimame kwenye nafasi yake ili malengo ya serikali yatimie.

“Chamwino iko kwenye mpango tangu mwaka 2018 lakini wengi bado wako kwenye mpango, tunataka matokeo chanya zaidi,” alisema

Washiriki wa mafunzo hayo,Salum Makila na Neema Joseph walisema watatekeleza wajibu wao vuizuri ili kuhakikisha walengwa wa mpango wananufaika.

Chanzo: www.habarileo.co.tz