Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC apiga marufuku watoto wenye utapiamlo kupelekwa kwa waganga wa kienyeji

Mbo1 Ed.jpeg DC apiga marufuku watoto wenye utapiamlo kupelekwa kwa waganga wa kienyeji

Sat, 4 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

MKUU wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amewaonya wazazi kuacha tabia ya kuwapelekwa watoto wenye utapiamlo kutibiwa kwa waganga wa kienyeji ambao hawana uwezo wa kutoa tiba hiyo na wanapozidiwa ndipo hukimbilia hospitali, huku watoto wakiwa tayari katika hali mbaya.

Mboneko amebainisha hayo leo, alipofanya ziara ya kutembelea kituo cha Afya cha Bugisi kilichopo Didia wilayani humo, na kuhamasisha akina mama wenye watoto walio na utapiamlo, ambao wanapatiwa matibabu kwenye kituo hicho kuzingatia lishe bora kwa watoto, pamoja na kuwanyonyesha maziwa ya kutosha.

Amesema baadhi ya wananchi wilayani humo, wakiwamo akina mama wenye watoto walio na utapiamlo wamekuwa na tabia ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kwenda kupatiwa matibabu badala ya kwenda Hospitali kwenye huduma sahihi na wanapozidiwa ndipo hukimbilia hospitali.

“Nimefanya ziara kwenye kituo hiki cha Afya Bugisi, nimepewa taarifa kuwa watoto wengi wenye utapiamlo ambao hufika hapa kupatiwa matibabu, wazazi wao huanzia kwanza kwa waganga wa kienyeji kutibiwa, na inaposhindikana ndipo wanawaleta hapa wakiwa tayari na hali mbaya,”

“Natoa wito kwa wananchi wote, acheni tabia ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kupatiwa matibabu, na msiwapeleke huko watoto wenu wenye utapiamlo, bali njooni kwenye huduma za afya mpate tiba sahihi na kuokoa afya zenu na watoto,” amesema Mboneko.

Aidha, amewataka pia akina mama kuzingatia suala la lishe bora kwa watoto wao  na kuwanyonyesha maziwa ya mama ya kutosha pamoja na wenyewe kula vyakula bora ili wapate maziwa mengi hali ambayo itawaepusha watoto kupata utapiamlo.



Naye, Daktari wa kituo hicho cha Afya Bugisi Zacharia Msumari, ambaye anahusika na masuala ya Lishe kwenye kituo hicho, amesema ndani ya miezi sita kuanzia Februari hadi Agost mwaka huu, walipokea watoto wenye utapiamlo 73, ambapo wengi walianzia kwa waganga wa kienyeji kupatiwa matibabu.

Amesema watoto hao wengine walifika hawana fahamu kabisa, pamoja na kuvimba mwili mzima, na wakawapatia matibabu, ambapo mpaka sasa wameshabakiwa na watoto Wanne ambao ndiyo wanaendelea kutibiwa, huku wengine wakiruhusiwa kwenda nyumbani.



Nao baadhi ya akina mama wenye watoto walio na Utapiamlo akiwamo Yunis Joseph kutoka Lyabukande wilayani humo amesema, mtoto wake alimfikisha hospitalini hapo kutoka kwa waganga wa kienyeji akiwa hali mbaya, lakini kwa sasa ana afya njema.
Chanzo: ippmedia.com