Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC apiga marufuku wananchi kuzaliana hovyo

Kalisdd DC apiga marufuku wananchi kuzaliana hovyo

Wed, 17 Nov 2021 Chanzo: Nipashe

MKUU wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Salum Kali, amepiga marufuku wakazi wa kisiwa cha Ijinga kilichoko ndani ya Ziwa Victoria kuzaliana bila utaratibu kwa kuwa hali hiyo itasababisha wakose eneo la kuishi.

Wakazi hao wapatao 2,800 wanaishi katika eneo lenye upana wa kilomita 8, na wanadaiwa kuzaliana kwa wingi kutokana na matumizi ya samaki aina ya ngele ambaye anachangia kuwapa hamu ya kujamiiana.

Mkuu huyo wa wilaya, alisema lazima kuwe na utaratibu maalum wa kuzaliana, na kwamba bila kufanya hivyo kisiwa hicho kitajaa watu na watakosa maeneo ya kulima na kujenga.

Akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho, katika uzinduzi wa tenki la maji lililojengwa kwa ufadhili wa Meya wa Jiji la Wurzburg, Kali alisema eneo hilo ni dogo na kwamba lazima kuwe na utaratibu la kuongeza idadi ya watu ili kuendana na nalo.

Alisema kijiji hicho ambacho kipo kisiwani, kimepitia wakati mgumu kwa muda mrefu kwa kukosa maji safi na salama na kwamba msaada huo umekuwa mkombozi kwao.

Aliwataka wananchi hao kutunza mradi huo wa maji ambao umegharimu Sh. milioni 275 ambao una uwezo wa kusambaza maji katika vijiji sita katika kisiwa hicho.

Aliongeza kuwa kipindi cha nyuma wananchi wengi waliugua ugonjwa wa kichocho kutokana na kukosa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi na kwamba kwa sasa tatizo hilo litabaki kuwa historia.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo wa maji, Meya wa jiji la Wurzburg nchini Ujerumani, Christian Schuchardt, alisema gharama za mradi huo zinafikia Sh. milioni 275.

Alisema fedha hizo ni michango ya wananchi wa jiji hilo nchini mwake ambazo zilichangwa ili kunusuru afya za Watanzania.

Aliwataka wananchi hao kutunza mradi huo ili uendelee kuwasaidia katika kupata maji safi na salama katika kipindi chote.

Meya huyo aliyekuwa ameambatana na ujumbe wake kutoka Ujerumani, alisema wakazi wa eneo hilo kwa kipindi kirefu walikuwa wakisumbuliwa na ugonjwa wa kichocho kutokana na kunywa maji ya ziwa yasiyo salama.

Chanzo: Nipashe