Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC apiga marufuku mikesha kwa watoto

6cee0cd4670a0759cd56761b3c8c8ed6 DC apiga marufuku mikesha kwa watoto

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mkuu wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Anna Gidarya amepiga marufuku mikesha ya makanisa kwa watoto wadogo ili kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji na ukatili uliokithiri wilayani humo kwa upande wa watoto wa kike.

Alitoa agizo hilo juzi wakati wa ziara yake ya kupokea kero za wananchi katika vijiji vya Ishinga Kata ya Ndola na Sapanda Kata ya Ngulilo.

Alisema mikesha mingi ya makanisa inayofanyika katika wilaya hiyo imekuwa miongoni mwa chanzo cha watoto wa kike kufanyiwa vitendo vya ukatili usiku hasa ubakaji na kusababisha ongezeko la mimba za utotoni.

Gidarya alisema kuwa vitendo vya ukatili kwa watoto vinaongezeka wilayani humo huku mikesha ya makanisa inayohusisha watoto ikishamiri siku hadi siku hali inayofanya baadhi yao kutumia nafasi hiyo kushawishiwa kushiriki vitendo viovu.

"Baadhi ya watu wenye nia ovu wamekuwa wakitumia mwanya huo wa mikesha kuwalaghai na kuwabaka watoto na kuwasababishia mimba za utotoni na kuharibu kabisa ndoto za maisha kwa watoto wa kike.

“Tuna taarifa za kutosha kuhusu watoto kufanyiwa ukatili na baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa makanisa, naombeni kila mtu achukue jukumu la kumlinda mtoto wa kike, vitendo hivi havivumiliki kabisa,” alisema.

Gidarya aliwaagiza viongozi wa vijiji vyote na kata zote kuhakikisha wanawachukulia hatua na kutoa taarifa za wazazi na walezi watakaokiuka na kuruhusu watoto wao kuhudhuria mikesha hiyo ya usiku.

Pia aliahidi kuwachukulia hatua viongozi wote wa vijiji na kata ambao watashindwa kudhibiti mikesha kwa watoto.

Sanjari na hilo, Mkuu wa Wilaya aliwahimiza wananchi wa Kata ya Ngulilo kubadilika na kuwapeleka watoto shule ili wakapate haki yao ya msingi kwa kuwa serikali imejikita kuboresha miundombinu ili kuimarisha mazingira ya kujifunza.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Sapanda, Elias Elijesel aliwataka wenyeviti wa vitongoji kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kukemea watoto wadogo kuzurura kwenye vilabu vya pombe usiku kwani ni chanzo cha kuibuka vitendo vya unyanyasaji.

Chanzo: www.habarileo.co.tz