Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC apiga marufuku michango ya madarasa

Kutongaaa DC Kanoni aagiza wananchi kutochangishwa ujenzi vyumba vya madarasa

Wed, 3 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe (DC) Lauter Kanoni ameagiza wananchi kutochangishwa katika kipindi hiki ambacho Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.

Agizo ameagiza wakati alipoungana na wananchi wa kijiji cha Igosi katika kuchimba msingi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Igosi iliyopo wilayani humo.

Amesema kazi ya wananchi katika kipindi hiki ni kusaidia kukusanya mawe, mchanga, matofali ambapo magari yatafika maeneo hayo kwa ajili ya kusombelea.

Amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule mbalimbali ikiwemo Sekondari ya Igosi.

"Wananchi wasitozwe fedha kwenye miradi hii, hiyo mingine ambayo tunapanga taratibu zetu za kuchangishana utaratibu huo utaendelea baadaye" amesema Kanoni.

Amesema ifikapo Desemba 20 mwaka huu kila shule ambayo ilipokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa inatakiwa kukamilisha ujenzi huo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe, Mariam Muhaji amesema fedha ambazo zimepelekwa wilayani humo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ni Sh1 bilioni.

Amesema kiasi hicho cha fedha kitaweza kujenga vyumba hamsini vya madarasa ambapo shule saba za msingi na kumi na tatu zimenufaika na mradi huo.

"Shule ya Sekondari Igosi ni mojawapo imepata ujenzi wa madarasa mawili ambayo gharama yake ni Sh40 milioni hii ni pamoja na nguvu ya wananchi" amesema Mariam.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kusogeza vifaa vya ujenzi na kuchimba msingi kwa ajili ya kusimamisha kuta za madarasa akiwemo Edina Mdemo na Erenesto Msemwa wamesema wamelazimika kuwekeana ratiba kwa kila kitongoji ili kukamilisha mradi huo kwa kuwa watoto wao wamekuwa na changamoto kubwa sana ya msongamano shuleni hapo.

"Kama wazazi tumewiwa kutoa nguvu zetu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na mabweni ili watoto wetu wasome katika mazingira mazuri" amesema Edina.

Chanzo: mwananchidigital