Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC aonya wachimbaji wa madini

991a944ebe8da8325eb78d1b5dc1d666 DC aonya wachimbaji wa madini

Thu, 8 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Kissa Gwakisa amewaonya wachimbaji wa madini wenye tabia ya kutorosha madini na kuuza nje ya nchi kinyemela waache mara moja, badala yake wafuate taratibu zilizowekwa na serikali.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa kufungua kituo cha uuzaji madini ya vito katika eneo la Kalalani wilayani Korogwe mkoani Tanga, ambapo alisema serikali imeweka utaratibu maalumu wa namna ya kuuza kwa kuweka vituo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Alisema licha ya utaratibu huo kuwepo lakini bado kuna watu wachache ambao wamekuwa walitumia njia zisizo rasmi kwa kutorosha madini na kwenda kuyauza nje ya nchi.

"Labda niwaambie kwamba Mkuu wa Polisi Wilaya ya Korogwe (OCD) ndio atakuwa na jukumu la kulinda kituo hiki kipya ambacho kinaanzishwa hapa cha ununuzi na uuzaji pamoja na jeshi la akiba watoe vijana kila siku ya soko ambao watakuja kuwasindikiza wanunuzi mpaka watakapotoka nje ya wilaya hiyo na ndio maana kamati ya ulinzi ipo hapa,"alisema.

Aidha alibainisha kwamba kwenye wilaya hiyo wana jumla ya leseni za wachimbaji 153 lakini zinazoonekana kufanya kazi ni 25, hivyo uanzishwaji wa kituo hicho utakuwa ni kuchochea cha wale wenye leseni ambazo hawafanyi kazi kufanya kazi ili leseni hizo ziweze kuleta tija kwa wananchi wa wilaya ya Korogwe na wanunuzi.

"Lakini pia niwaambie kwamba tunafikiria kuanzisha kituo kikubwa Korogwe Mjini cha soko la madini, ni mipango wanaoendelea nayo na tunaamini utakuwa na tija hivyo kuwawezesha wachimbaji kuuza madini yao," alisema.

Awali akizungumza katika ufunguzi huo, Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu Napacho aliwataka wachimbaji wa madini kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria huku akieleza wadau wa kalalani watauza madini yao hapa hapo kwenye kituo hicho.

Chanzo: habarileo.co.tz