Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC amshukuru JPM kwa kutengua uteuzi wake

40893 Pic+jpm DC amshukuru JPM kwa kutengua uteuzi wake

Tue, 12 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Aaron Mbogho amemshukuru Rais John Magufuli kwa kumtenganisha na watu aliodai wameshindwa kuelewana kimtizamo.

Mbogho alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wake kwa maelezo ya kutoelewana na wafanyakazi wenzake.

Alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wa kumuondoa kwenye nafasi hiyo kwa sababu amemsaidia kutokutenda dhambi ya kudhalilisha mamlaka ya uteuzi kwa kujiuzulu mwenyewe.

“Nilikokuwa nimefikia nilikuwa navumilia sana taabu ya kufanya kazi na watu ambao wana mitazamo kinzani.

“Ninachokiona ni sita, wao wanakiona ni tisa kwa sababu wamesimama ambako hawatakiwi kusimama ili kuisoma hiyo namba kwa sababu ya kujali masilahi binafsi wakati mimi naangalia masilahi mapana kwa ajili ya manufaa ya Taifa,” alisema.

Alisema wengi wa watendaji lengo lao ni kufaidika kutokana na kila wanachofanya, badala ya kufikiria namna jamii itakavyonufaika na utendaji wao wa kazi.

“Kuitwa mkali ama mnoko kwa masilahi ya taifa ni jambo jema kuliko kuitwa mkarimu na mpole kwa upendeleo na woga wa kuchukua maamuzi ili kuilinda nafasi yangu,” alisema.

Mbogho ambaye anajivunia kuongeza mapato ya halmashauri kutoka chini ya bilioni moja kwa mwaka hadi zaidi ya Sh3 bilioni, alisema alilazimika kuwaweka watu ndani wakiwamo watumishi wa Serikali kutokana na matendo yao yaliyohusiana na uhalifu.

“Kwa kifupi, wote nilioamuru waende polisi ama wawekwe rumande walikuwa na makosa yaliyowapelekea kufikishwa huko, hakuna mtu ambaye niliamrisha apelekwe kisa ameniudhi mimi binafsi kwenye mambo yasiyo ya kikazi ama yasiyo na public interest (manufaa ya taifa),” alisema Mbogho.

Alichoeleza Rais Magufuli

Wakati wa hafla ya kuwaapisha majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani ambayo ilihudhuriwa pia na wakuu wawili wa wilaya za Mwanga na Tarime waliokuwa wameteuliwa, Rais Magufuli alieleza sababu za kumuondoa Mbogho.

“Akiwa wilayani Mwanga yaliyokuwa yanatokea wote tumesikia, viongozi wamewekwa ndani na unapofuatilia unaona chanzo ni yeye. Katika mazungumzo yake amekuwa akisema kuwa yeye ndio mtalaamu wa wadudu peke yake nchini Tanzania.

“ Hivyo huenda na watu nao anawaona kama wadudu, hivyo nimeona kwa kuwa ni mtalaam katika eneo hili basi acha aende huko akachunguze vizuri wadudu,” alisema Rais Magufuli.

Mahojiano zaidi soma ukurasa wa 21.



Chanzo: mwananchi.co.tz