Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC amjibu msukuma sakata la machinga

Msukuma Hj Mbunge Joseph Kasheku

Sat, 4 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanza. Wakati Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku 'Musukuma' akieleza kutoridhishwa na mchakato wa kuwaondoa Machinga katika maeneo yaliyokatazwa, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala amesema lengo la Serikali siyo kuwafilisi bali kuwajengea miundombinu rafiki ya biashara yao.

Masala ametoa majibu hayo katika maadhimisho ya miaka 46 ya kuanzishwa kwa CCM yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza kufuatia mbunge huyo ambaye awali amedai kuwa Rais, Samia Suluhu Hassan aliagiza Machinga wapangwe siyo kufilisiwa kwa ilivyotokea kwa baadhi ya wafanyabiashara hao.

Mkuu huyo wa wilaya amekanusha taarifa ya Machinga kupigwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima huku akisema waliofanyiwa hivyo ni walioshindwa kutii maelekezo waliyopewa.

"Serikali inajali na haipo kuua mitaji wala kuwadidimiza hao wafanyabiashara hata kwenye kuwahamisha hajapigwa mfanyabiashara yoyote, wachache ambao wamefanyiwa hivyo ni pale waliposhindwa kutii maelekezo waliyopewa," amesema Masala.

Amesema kabla ya kuanza kuwahamisha, serikali ilikaa kikao na viongozi wao wakapendekeza masoko wanayohitaji kuhamishiwa ambapo walibainisha masoko nane wilayani Ilemela na masoko zaidi ya saba wilayani Nyamagana.

"Hakuna nchi inayoishi bila kuweka utaratibu mzuri wa wafanyabiashara wake kufanya kazi katika mazingira mazuri, tumekaa na viongozi wao na hapa wapo jukwaani hii ni kuonyesha kwamba wanaunga mkono juhudi za serikali kuwaboreshea mazingira ya biashara," amesema.

"Tulikaa nao wakasema wanataka miundombinu ya aina gani katika soko la Kabwalo, Sabasaba, Pansissi, Kiloleli na Buzuruga na yote yameboreshwa. Hauwezi kuwa na sehemu moja itakayohudumia wakazi wengi wa mkoa huu bali kutenga masoko mbalimbali kama tulivyofanya," amesema.

Amesema katika kuhakikisha kunakuwa na soko katikati ya jiji, Serikali inakamilisha ujenzi wa Soko la Mwanza mjini kwa gharama ya Sh16 bilioni ambapo linatarajiwa kukamilika mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live