Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC ahamishia shuleni familia zilizokumbwa na mafuriko

SABAYA DC ahamishia shuleni familia zilizokumbwa na mafuriko

Sat, 25 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAYA 44 zimezingirwa na maji, huku familia 13 zikiwa katika hali mbaya wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, kutokana na mafuriko makubwa yaliyoikumba.

Kutokana na baa hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya, amezihamishia kwa muda katika majengo ya Shule ya Msingi Sanya Station iliyoko Kata ya Kia kaya sita ambazo zina idadi kubwa ya watoto.

Jana, Ole Sabaya alisema: “Mpaka sasa tumefanikiwa kuzihamishia familia hizo shuleni, hali ni mbaya na kimsingi walio katika mahangaiko kutokana na mafuriko haya yanayotokana na mvua ya masika inayoendelea kunyesha kuzingira makazi yao, ni familia 44.

Kati yao, familia 13 ndiyo ambazo ziko kwenye hali mbaya na hawana kabisa makazi. Hili ni janga la asili, ndiyo maana nimesaidiana na maofisa wangu kuchukua hatua haraka kunusuru maisha ya wananchi," Ole Sabaya alisema.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya familia kuyakimbia makazi yao na kutafuta hifadhi katika vitongoji vya jirani ili kuokoa maisha yao.

Kwa mujibu wa Ole Sabaya, familia zote zinazopambana na mafuriko hayo yanayotokana na janga la asili, zitahamishiwa maeneo salama ikiwamo kupata hifadhi kwa majirani zao.

Akizungumza na waathirika wa mafuriko hayo, Mkuu wa Wilaya huyo alisema kazi inayoendelea ni kufungua maji ya mafuriko na kuyaelekeza kwenda Mto Kikuletwa, kwa kuwa maji hayo yanayojaa eneo la Sanya Station kutokea milimani, yanatokana na wananchi kujenga eneo la asili ya maji.

Ofisa Kilimo wa Kata ya Kia, Maurin Mushi, akizungumzia mafuriko hayo, alisema zaidi ya ekari 175 za mazao mbalimbali, yakiwamo maharagwe, pilipili hoho na mahindi, zimeharibiwa vibaya kwa mazao hayo kusombwa na maji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live