Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC aambiwa unyago unafundisha heshima jamii

49452 Pic+unyago

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ruangwa. Wakati unyago ukipigwa vita kutokana na madai kuwa unachangia kuharibu watoto wa kike, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Hashim Mgandilwa ameelezwa umuhimu wa mila hiyo.

Aliambiwa maneno hayo wakati wa kikao cha wadau wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kilichojadili mila na desturi zinazochochea ukatili kwa wanawake na watoto.

Abdallah Mbinga, mkazi wa kijiji cha Likunja ambaye anamiliki kiwanja kinachotumika kufundishia unyago watoto wa kuanzia umri wa miaka mitano, ndiye aliyejitwisha mzigo huo wa kuelezea umuhimu wa mila hiyo inayoonekana kuharakisha wasichana wadogo kujua masuala ya mahusiano.

Mbinga alisema hakuna kibaya wanachofundishwa watoto zaidi ya kuwa na heshima katika jamii.

DC: Je, watoto wanaochezwa unyago ni wa umri gani?

Mbinga: Ni wa umri wa miaka mitano mpaka sita.

DC: Wanafundishwa nini wanapokuwa katika mafunzo hayo?

Mbinga: Wanafundishwa heshima na wengi wanakuwa bado hawajaanza shule kwa sababu ni wale wenye umri wa miaka minne, mitano hadi sita.

DC: Unaweza kuniambia mada wanazofundishwa watoto wa kike na wa kiume katika unyago?

Mbinga: Wanafundishwa heshima. Watoto wanaochezwa unyago wanakaa kwa siku 18 hadi 20 na mila hizo zinafanyika wakati wa likizo tu.

Lakini DC Mgandilwa alisema baada ya mahojiano hayo kuwa anaamini moja ya miiko ya unyago ni kutotoa siri ya kile kinachofundishwa.

Akizungumzia mila hizo, mganga mkuu wa wilaya, Godfrey Njile alisema ni muhimu viongozi wa Serikali wakajua kwa undani nini kinachofundishwa katika mila za unyago.

Alisema ni vizuri ukafanyika utafiti kujua kwa nini unyago unapendwa zaidi na pia mada zinazofundishwa.

Akizungumzia masuala ya unyago, mkazi wa Likunja, Leticia Ng’ombo alisema tatizo katika jamii liko kwa kinamama ambao wana madaraka makubwa kuliko waume zao.

“Hata baba anapomkanya mtoto kuhusu maadili, mama anakuja juu na hivyo kusababisha mtoto wa kike kuendelea kuharibika,” alisema Ng’ombo.

Alisema wapo watoto wa miaka miwili wanaotakiwa kupelekwa kliniki, lakini wanapelekwa kuchezwa unyago.

Akizungumzia suala hilo, mkuu wa dawati la jinsi wa polisi, Upendo Komba alisema: “Tulibaini kuwa wale wanafunzi (wanne) walibakwa kutokana na kile wanachofundishwa kwenye unyango kwa sababu tulipowahoji walisema wanafundishwa kukata kiuno.”



Chanzo: mwananchi.co.tz