Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC aagize walimu wanaofaulisha masomo kiwilaya kupewa viwanja

Nguvila.jpeg DC aagize walimu wanaofaulisha masomo kiwilaya kupewa viwanja

Mon, 23 Aug 2021 Chanzo: Nipashe

MKUU wa Wilaya ya Muleba Thoba Nguvila, ameagiza walimu ambao masomo yao yataongoza kiwilaya katika mitihani ya Taifa ya darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita kupewa zawadi ya viwanja kama motisha, badala ya kuwaandikia barua za pongezi tu, lengo likiwa ni kuhakikisha ufaulu unaongezeka.

Mkuu huyo wa Wilaya ametoa kauli hiyo wakati akikabidhiwa matanki nane ya kuvunia maji ya mvua, matundu 24 ya vyoo na vyumba vinne vya madarasa, vilivyojengwa na shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Kagera kupitia miradi wa Ruhita AP na Mbuka AP kwa gharama ya shilingi milioni 305.1.

Nguvila amesema ili kutimiza azma hiyo mwaka huu wanatenga viwanja tisa kwa ajili ya walimu ambao masomo yao yatashika nafasi ya kwanza hadi ya tatu, na kwamba hatua hii itawafanya walimu kuwa na ushindani katika ufundishaji.

"Walimu hatuwezi kuendelea kuwa na zawadi ya kuwaandikia barua tu za pongezi kwamba hongera mwalimu, ina maana akiongoza mara 30 ajaziwe barua 30 ofisini, kwani atakula barua, lakini mwalimu akiwa na kiwanja na kujenga nyumba ni kumbukumbu nzuri kwake na kwa familia yake kuwa alifanya kazi nzuri" amesema.

Akikabidhi miundombinu hiyo na matanki ya maji vilivyonufaisha shule za msingi tisa ambazo ni Nyakatanga, Kishuro, Burungura, Mtulange, Nyarugando, Kakoma na Nyakishozi zilizoko chini ya mradi wa Ruhita AP na Kangoma na Bushekya zilizoko chini ya mradi wa Mbuka AP, mkurugenzi wa rasirimali watu wa shirika hilo Joan Kiiza amesema kuwa lengo ni kupunguza msongamano darasani na kulinda afya za wanafunzi.

"Kati ya shilingi milioni 183.1 zilizotumika kununua matanki ya maji, kutengeneza miundombinu ya maji na kujenga matundu 24 ya vyoo katika shule saba za msingi chini ya mradi wa Ruhita AP, wananchi walichangia shilingi 840,000" amesema.

Aidha amesema katika ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa vilivyojengwa katika shule mbili za Kangoma na Bushekya kupitia mradi wa Mbuka AP kwa gharama ya shilingi milioni 122, wananchi walichangia shilingi 655,000.

Baadhi ya walimu waliozungumza kuhusiana na motisha hiyo akiwamo Christopher Lenard wa shule ya msingi Burungura wamesema itasaidia kuongeza ufaulu maana kila mwalimu atapambana ili somo lake liongoze, na kuishukuru World Vision kwa kuendelea kuboresha miundombinu katika shule ambayo pia huchangia watoto kufaulu.

Chanzo: Nipashe