Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC aagiza viongozi 52 wa Amcos wakamatwe kwa ubadhirifu

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maswa. Mara kadhaa Rais John Magufuli amekaririwa akionya kuwa fedha za umma ni sumu na anayezitafuna atazitapika kwa njia yoyote ile.

Onyo hilo linaonekana halikuwafikia baadhi ya viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (Amcos) wilayani Maswa mkoani Simiyu ambao kwa sasa 52 kati yao wanatuhumiwa kukopeshana na kutafuna isivyo halali zaidi ya Sh30 milioni kati ya fedha walizokabidhiwa kwa ajili ya ununuzi wa pamba.

Akizungumza wakati wa mkutano wa wajumbe zaidi ya 400 wa vyama vya ushirika vya msingi wilayani humo, Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Seif Shekalaghe aliagiza kukamatwa kwa viongozi hao 52 wa vyama vya ushirika wilayani humo wanaotuhumiwa kujikopesha fedha hizo kinyume cha sheria.

“Ninachotaka ni fedha zilizopotea zipatikane; iwe kwa wahusika kuuza ng’ombe au mali zao hilo mimi silijui. Na hii ni hatua ya mwanzo kwa sababu uhakiki wa kina bado unaendelea,” alisema Dk Shekalaghe.

Wilaya ya Maswa ina jumla ya vyama vya msingi vya ushirika 120 ambavyo baadhi ya viongozi wake wanatuhumiwa kujikopesha kinyume cha sheria fedha za ushirika walizokabidhiwa kwa ajili ya kununulia pamba.

Msimu uliopita, shughuli ya kununua pamba ilifanyika kupitia vyama vya msingi vya ushirika baada ya Serikali kufuta mfumo wa awali wa kazi kufanywa na kampuni binafsi ambazo baadhi huingia mikataba na wakulima.

Katika hatua nyingine, Dk Shekalage aliagiza kusimamishwa kazi kwa Ofisa Ushirika wa Wilaya ya Maswa, George Budodi kwa tuhuma za kushindwa kutekeleza wajibu wake hadi kuifanya ofisi ya mkuu wa wilaya kuingilia baadhi ya shughuli alizopaswa kuzifanya.

Muda mfupi kabla ya kusimamishwa kazi, Budodi pia aliutumia mkutano huo kuwaonya baadhi ya viongozi wa Amcos wilayani humo kuacha tabia ya kuuza mbegu ya pamba inayotolewa bure na Serikali.

Mmoja wa viongozi wa Amcos aliyehudhuria kikao hicho, Eveline Subiaga aliwasihi wenzake kuwa waadilifu katika kusimamia vyama vyao kwa mujibu wa sheria ili kuepuka kuishia kwenye mikono ya dola.



Chanzo: mwananchi.co.tz