Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC aagiza kuondolewa kwa korosho chafu ghalani

3f66faba5e9a553c178b67204d6c03f4 DC aagiza kuondolewa kwa korosho chafu ghalani

Sun, 4 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai ametaka vyama vya ushirika vya msingi vya mazao (Amcos) 11 vilivyoshiriki katika kuingiza korosho chafu katika ghala kuu la Nangurukuru kwenda kuondoa korosho zao.

Korosho hizo ni za msimu wa 2019/2020.

Aidha alisema kuanzia msimu huu wa 2020/2021 chama chochote kitakachoingiza korosho chafu katika ghala viongozi wa vyama hivyo na wakulima husika watafunguliwa mashtaka.

Alisema kauli hiyo wakati akizungumza na wanachama wa chama cha ushirika wa kuuza mazao (Amcos) cha Kinjumbi , wilayani hapa ambao wamekuwa wakilalamika kwamba korosho tajwa si zao.

Ngubiagai alisema wakati wilaya hiyo ikijiandaa na mavuno ya ufuta, maghala husika ni lazima yawe wazi na masafi kwa hiyo ni lazima wahusika waondoe korosho hizo haraka na kwenda kuziteketeza kwa kuwa hazifai kwa matumizi.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya kuna tani 100 za korosho chafu ambazo hazifai kwa matumizi na miongoni mwa vyama vinavyohusika ni Kinjumbi wenye tani 19.5 sawa na magunia 259. Vyama vingine ni pamoja na Pande, Somanga na Matandu.

Alisema wakati uzalishaji wa korosho katika wilaya hiyo ni tani 5,000 kuwa na tani 100 za korosho chafu si kitu kizuri katika uimarishaji wa masoko ya bidhaa kutoka wilayani humo.

Ngubiagai alisema katika korosho hizo chafu katika kilo unapata korosho angalau nne hadi tano na kwamba wilaya na uongozi hautavumilia uhujumu uchumi wa wilaya hiyo wa kiwango hicho.

Alisema pamoja na kuwataka wahamishe korosho hizo na kwenda kuziteketeza, kitendo cha kuendelea kuweka korosho hizo ghalani zitawaletea wahusika deni kubwa ambalo linaweza kuwafanya watawanyike na kuvunja vyama vyao.

Kwa mujibu wa taratibu za maghala wilayani Kilwa kila kilo moja ya korosho hutozwa Sh 100 kwa siku inapokuwa ghalani.

Alisema vyama hivyo vinatakiwa kwenda kuondoa korosho hizo kwa kuwa muda umeisha na kwamba chama kikuu lazima kianze kujiandaa kwa msimu wa ufuta.

Chanzo: www.habarileo.co.tz