Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC aagiza kukamatwa watumishi tisa soko Kwa Sadala kwa tuhuma za ubadhirifu

21272 Dc+pic TanzaniaWeb

Mon, 8 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hai. Mkuu wa Wilaya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ameamuru  kukamatwa watumishi tisa wa soko la Kwa Sadala la wilayani humo akiwamo mkuu wa soko hilo, Joseph Akyoo kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo hilo jana baada ya kupokea malalamiko ya wafanyabiashara wa soko hilo, kupewa risiti za kugushi na kutokutumika risiti za mashine za EFD katika kukusanya mapato.

Mkuu huyo wa wilaya aliagiza maofisa wa taasisi za kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) na maofisa wa polisi waliokuwapo katika mkutano wa kusikiliza kero za wafanyabiashara wa soko hilo, kuwakamata maofisa hao ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

Sabaya amesema katika kipindi kifupi, amebaini katika soko hilo kuna upungufu mkubwa katika makusanyo wa fedha hivyo kuna dalili za ubadhilifu wa fedha za umma.

"Soko hili licha ya kuwa na wafanyabiashara wengi wa ndani na nje ya nchi lakini, bado mapato ni madogo na nakubaliana na wafanyabiashara kuna mchezo mchafu hapa ambao lazima uchunguzwe," amesema.

Awali, wakizungumza katika mkutano huo, wafanyabiashara wa soko hilo, Erick Ndosi na Amina Abdalah wamesema wamekuwa wakipewa risiti za mikono ambazo nyingi ni za kutengenezwa mitaani.

Ndosi amesema licha ya kupewa risiti za mkono ambazo hawaamini kama fedha zote zinafika halmashauri pia soko hilo ni chafu na hivyo hawajui fedha zinafanya kazi gani.

Amina amesema viongozi wa soko hilo wamekuwa wakitoza  ushuru mkubwa na kutoa risiti ambazo sio za halmashauri hivyo kuomba uchunguzi wa tukio hilo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai, Yohana Sinto amesema halmashauri hiyo itafuatilia kama ni kweli mashine hizo zimeharibika au zimeharibiwa na maofisa hao kwani ni makosa kutumia risiti zisizo za EFD.

Chanzo: mwananchi.co.tz