Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC aagiza kukamatwa wanaobariki ndoa za watoto darasa la 7

8c1d13ed88b94a9a7d93cd6c8c00fe1c DC aagiza kukamatwa wanaobariki ndoa za watoto darasa la 7

Mon, 13 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Geita mkoani hapa, Wilson Shimo ametoa onyo kwa walezi na wazazi watakaodiriki kubariki ndoa za watoto waliohitimu elimu ya shule ya msingi na kuwazuia kuendelea na masomo ya sekondari.

Alitoa onyo hilo juzi alipokua akiweka jiwe la msingi Katika Shule ya Sekondari Royal Family.

Alitumia fursa hiyo pia kuwakumbusha wazazi wajibu wa kuendeleza watoto wanapofaulu kujiunga na elimu ya sekondari.

“Atakayekaidi kwa makusudi atawajibishwa kwa mujibu wa sheria. Wahitimu wa shule za msingi ni watoto wadogo sana wanaopaswa kuendelezwa kielimu, kiakili na kimalezi hadi kutimiza ndoto zao na kuongezea taifa wataalamu, wajuzi na wabobezi wa fani mbalimbali,”alisema.

Alitoa pia rai kwa taasisi binafsi kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuongeza wigo wa ushindani wa kielimu na kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali kukuza sekta hiyo.

Meneja wa Shule za Royal Family, Razaro Philipo alisema sera rafiki za serikali ndio zimeshawishi kuwekeza katika sekta ya elimu, akaahidi kuendelea kuzalisha wahitimu waliotukuka kwa manufaa ya taifa.

Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Wilaya, Cosmas Fortunatus alisema uzinduzi wa shule hiyo unafanya jumla ya shule za sekondari za taasisi binafsi kufikia nane, akawasihi wawekezaji wengine kupata fursa katika sekta hiyo.

Alisema kwa ujumla wake, shule za sekondari (serikali na binafsi) ni 27 kwa Halmashauri ya Mji wa Geita, alisema: “Hii ni kudhihirisha kukua kwa sekta ya elimu katika wilaya yetu na nchi kwa ujumla. Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, wadau wajitikeze kukamata fursa”.

Chanzo: www.habarileo.co.tz