Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amemwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo kuanza doria nyakati za usiku katika stendi ya mabasi Same mjini, ili kuwabaini na kuwakamata wanaotumia stendi hiyo kufanya mambo yasiyo na maadili.
Amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakilitumia eneo hilo la stendi vibaya na kwamba kila siku zimekuwa zikikutwa kondomu zilizotumika zimezagaa ndani ya stendi hiyo.
Mgeni ametoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika katika viwanja vya stendi hiyo, wakati akisikiliza kero mbalimbali za wananchi wa wilaya hiyo.
"Hili eneo la stendi kuna watu wanalitumia vibaya sana, tunakumbana na kondomu kila siku hapa stendi, kuna kitu gani kinafanyika hapa, OCD nikuombe fanya doria kamata wote weka ndani uwachukulie hatua kwa mujibu wa sheria," amesema DC Mgeni.
Ameongeza: "Wanatuharibia sana watoto wetu hapa Same, mimi kama mkuu wenu wa wilaya na mwakilishi wa Rais katika wilaya hii ya Same na kama mwanamke, nina uchungu sana na hawa watoto, niwaombe sana wazazi timizeni wajibu wenu,"
"Sitaki kusikia tena kuna kondomu hapa, na kila mzazi awe mlinzi wa mwenzake hata kama mzazi unaona yule mtoto sio wa kwako anarandaranda maeneo ya hapa stendi nyakati za usiku, mtoto wa mwenzake ni wa kwako, mweleze mzazi mwenzako usione kama una kiherehere unakuwa umeokoa taifa la kesho,"
Pamoja na mambo mengine, amesema atahakikisha wazazi wote ambao hawawajibiki kwa watoto wao wanachukuliwa hatua za kisheria.
" Nikuombe OCD mnapofanya doria za usiku mnapokamata hawa watoto, naomba hakikisheni mnaita wazazi na muwahoji ni kwa nini hawawajibiki kwa watoto wao, ili sheria ichukue mkondo wake,"amesema.
Elisa Mdee, mmoja wa wananchi wa Same, amesema suala la utupaji wa kondomu kiholela katika stendi hiyo, limekuwa ni kero kubwa hasa kwa watoto wanaopita na kukuta zimezagaa ovyo katika maeneo hayo.
"Hali hii inatupa fedheha kubwa, maana inatoa picha mbaya kwa watoto wetu hivyo tunaomba vyombo vinavyohusika na hili vichukue hatua ili kunusuru watoto wetu hawa, maana haileti picha nzuri kwa jamii," amesema Elisa.
Naye, Amir Mgonja, mkazi wa Same mjini amesema endapo serikali ingeweka taa katika stendi hiyo kusingekuwa na mambo hayo ya ovyo ambayo yanafanyika nyakati za usiku katika eneo hilo.
"Eneo letu la stendi lingekuwa na taa sidhani kama yangefanyika haya ambayo yanafanyika hapa nyakati za usiku. Tunaomba mamlaka zinazohusika zichukue hatua, maana hii ni fedheha sana, watoto wetu kupita hapa na kukuta kondomu zilizotumika sio sawa,"amesema.