Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Tarime alivyomuokoa kijana aliyefanyiwa tohara

Wed, 12 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tarime. Mkuu wa wilaya ya Tarime,  Glorious Luoga  amelazimika kutumia nguvu kumchukua kijana mmoja na kumkimbiza hospitali ya Wilaya ya Tarime kutokana na kutoka damu nyingi saa chache baada ya kufanyiwa tohara.

Amechukua uamuzi huo leo Jumatano Desemba 12, 2018 baada ya ndugu wa kijana huyo kukataa wazo la mkuu huyo wa wilaya aliyekuwa akipita katika kijiji cha Kemakorere na kumkuta akiwa ameketi chini akitokwa na damu nyingi na kuishiwa nguvu.

Luoga alikuwa akielekea katika kijiji cha Nyamongo kushiriki kikao lakini alilazimika kuahirisha kwa muda safari yake na kuwapigia simu polisi kufika eneo hilo kumchukua kijana huyo kwa ajili ya kumpeleka hospitali.

Ndugu wa kijana huyo walimjibu Luoga kuwa hali ya kijana wao kuishiwa nguvu ni ya kawaida, hasa kwa anayetoka kufanyiwa tohara na kulingana na mila hapaswi kupelekwa hospitali.

Luoga amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakizuia tohara zisizokuwa salama lakini baadhi ya watu hupinga.

Amesema Serikali haizuii tohara lakini lazima zifanyike katika mazingira salama.

Akizungumza baada ya kumpokea kijana huyo, daktari wa zamu hospitali ya wilaya Tarime, Devotha Ernest amesema walimpokea akiwa katika hali mbaya.

Amesema hakuwa akijitambua na uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa amepoteza damu nyingi.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz