Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Simanjiro aeleza sababu kuvunja mkutano wa wamiliki wa migodi Mirerani

11833 MGODI TanzaniaWeb

Fri, 20 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mirerani. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara,  mhandisi Zephania Chaula amesema alivunja mkutano wa wamiliki wa migodi na wanunuzi wa madini ya Tanzanite baada ya kupata taarifa kuwa haukuwa na lengo zuri.

 

Mkutano huo uliopangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Luka katika mji mdogo wa Mirerani  kujadili namna ya kuingia katika eneo la mgodi wa madini wa Tanzanite lililozungushiwa ukuta, uliovunjwa jana Julai 19, 2018 na mkuu huyo wa wilaya.

 

Akizungumza leo Ijumaa Julai 20, 2018 Chaula amesema alipata taarifa kuwa kutaibuka vurugu, kuwaagiza polisi kuzuia mkutano huo.

 

Amesema awali polisi walitoa kibali kwa viongozi wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (Marema) kufanya mkutano huo.

 

“Wasubiri hizi siku mbili tatu hali itulie kisha wataruhusiwa kufanya mkutano wao ila kwa sasa wanapaswa kuheshimu maamuzi ya Serikali,” amesema.

 

Mwenyekiti wa Marema mkoa wa Manyara, Sadiki Mneney ameieleza MCL Digital kuwa walipewa kibali cha kukutana, kushangazwa na hatua za kuzuiwa kuendelea na mkuano huo.

 

Amesema lengo la kukutana kwao ilikuwa  kujadili changamoto wanazokutana nao wakati wa kuingia na kutoka katika mgodi huo.

 

"Hivi sasa kuna changamoto ya magari kuzuiwa kuingia na kutoka ndani ya ukuta unaozunguka migodi hiyo na wafanyakazi wetu wanatakiwa kuingia kwa kutumia vitambulisho vya Taifa na vya Wizara ya Madini na wengi wao hawana," amesema.

 

Mmoja kati ya wamiliki wa migodi ya Tanzanite, Abubakary Mwamba amesema Serikali inapaswa kutekeleza kwa vitendo kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati akizindua ukuta huo kuwa wachimbaji wasinyanyaswe.

 

"Sasa hivi hata maji katika migodi ni ya shida kwa sababu magari hayaruhusiwi kuingia wala kutoka ndani ya ukuta unaozunguka mgodi. Serikali inapaswa kuweka utaratibu mzuri tofauti na huu wa sasa,” amesema.

 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesema wamiliki wa migodi na wachimbaji wa madini wanapaswa kutii maagizo ya Serikali ya namna ya kuingia na kutoka ndani ya ukuta huo unaozunguka migodi ya Tanzanite.

 

Hivi karibuni Tume ya madini iliyoundwa na Rais John Magufuli, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Idris Kikula ilibaini utoroshwaji wa madini ya Tanzanite uliosababiaha mrabaha kushuka kutoka Sh444 milioni kwa mwezi hadi Sh40 milioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz