Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Rorya atuliza wananchi vijiji jirani shamba la mifugo Utegi

Oicha Utegi Data Baadhi ya wakazi wa vijiji sita vinavyopakana na shamba la mifugo la Utegi wilayani Rorya

Fri, 19 May 2023 Chanzo: Mwananchi

Serikali imewaondoa hofu wakazi wa vijiji sita vya Wilaya ya Rorya vinavyopakana na shamba la mifugo la Serikali la Utegi (Utegi Dairy Farm) kuwa kila mtu ambaye ardhi yake itatwaliwa na kuingizwa kwenye mradi wa kukufua shamba hilo atalipwa fidia stahiki.

Ahadi hiyo imetolewa leo Mei 19, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka alipozungumza na wananchi kutuliza hofu ya iliyotanda ya kutofahamu hatima ya maeneo na mashamba yao yanayotarajiwa kutwaliwa ili kuongeza uwekezaji na tija katika uendeshaji wa shamba hilo.

Shamba la mifugo Utegi lina ukubwa wa ekari 4, 400, kati ya hizo, ekari 400 zinadaiwa kuwa ni makazi ya watu, mashamba na malisho ya mifugo katika vijiji sita vya Utegi, Majengo, Mika, Omuga, Nyasoro na Ingri Chini.

Shamba hilo ambalo pia linamiliki kiwanda cha kuchakata maziwa imesitisha uzalishaji kwa zaidi ya miaka 30 sasa, hali inayoongeza uvamizi na shughuli za kibinadamu.

"Wataalamu wanatarajiwa kufika katika vijiji vyote sita kwa ajili ya tathmini ya maeneo yatakayotwaliwa kwa ajili ya uendelezaji wa shamba la mifugo Utegi. Nawasihi wananchi kuwa watulivu wakati kazi hii inayotarajiwa kufanyika ndani ya miezi miwili ijayo inakamilishwa,’’ amesema Chikoka

Wakitoa hoja zao mbele ya Mkuu wa Wilaya, baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nyasoro wamedai ukimya wa Serikali baada ya kutangaza nia ya kutwaa baadhi ya maeneo ya vijiji umesababisha hofu miongoni mwa wananchi kuhusu fidia.

‘’Wakazi wa vijiji vya Nyasoro, Utegi, Omuga, Mika, Majengo na Ingri Chini ambao maeneo yao yanaingia kwenye mradi wa shamba la mifugo Utegi wanashindwa kuendelea maeneo yao kutokana na tangazo la Serikali la kuyatwaa. Tunaomba suala hili lihitimishwe ili tuendelee na maisha mengine,’’ amesema Deus Nyambaso, mkazi wa Kijiji cha Nyasoro

Charles Opiyo, mkazi wa Kijiji cha Utegi amesema hofu ya wananchi imeongezeka baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anjelina Mabula kufika kijijini hapo Mei 7, 2023 na kusisitiza nia ya Serikali ya kutwaa maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji kwenye shamba la mifugo Utegi.

"Kimsingi, wananchi hatupingi nia ya Serikali ya kufufua shambal la mifugo Utegi kwa sababu mradi huo utatunufaisha pia vijiji jirani. Jambo tunaloomba ni fidia stahiki ikiwemo maeneo mapya ya makazi, kilimo na malisho kwa wote ambao ardhi zao zitatwaliwa kwa ajili ya mradi huu,’’ amesema Charles Opiyo

Amesema wananchi wameingiwa hofu zaidi baada ya kuona kundi la watu waliodaiwa kuwa ni wataalam waliofika katika maeneo ya vijiji wakiongozana na viongozi wa Serikali za mitaa na kuanza kupima na kusimika vigingi vya mpaka bila kuwashirikisha wananchi ambao baadhi wameisha maeneo hayo kwa zaidi ya miaka 70.

Akisistiza hoja hiyo, Kaimu Mtendaji wa Serikali ya Kijiji cha Nyasoro, Andrew Okoth amesema kitendo cha vigingi kuwekwa bila wananchi kushirikishwa ni kinyume cha ahadi ya Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rorya kuwa shughuli hiyo itashirikisha hatua kwa hatua kabla ya maeneo yao kutwaliwa.

Chanzo: Mwananchi