Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dk Linda Salekwa ameliagiza Gereza la Isupilo lililopo Wilayani hapa kuhakikisha wanatoa elimu ya majanga ya moto kwa wananchi wanaolima katika maeneo ya gereza hilo.
Gereza hilo limetoa baadhi ya maeneo yake na kuwaazima wananchi wanaozunguka eneo hilo kwa ajili ya shughuli ya kilimo huku changamoto ikitajwa ni kuibuka kwa moto katika mashamba hayo na kusambaa katika vijiji jirani jambo ambalo linaibua kero.
Dk Salekwa ameyasema hayo Jumapili Novemba 19, 2023 kwenye Mkutano wa hadhara baada ya kusikiliza kero za wananchi wa Kata ya Wambi kuhusu athari za moto hutoka katika maeneo ya gereza hilo na kuelekea katika mashamba ya wananchi.
"Jukumu la kuwafundisha wananchi ambao wanaolima kwenye maeneo yenu kuhusu majanga ya moto ni la kwenu kama ambavyo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia shamba la miti la Serikali Sao hill wanavyofanya,”amesema Dk Salekwa
Pia amewakata kutengeneza ‘fire lines’ katika ameneo yao ili kuhakikisha wanazuia moto huo usiweze kusambaza katika maeneo mengine na kuleta hasara kwa wananchi.
Pia, Dk Salekwa amewasisitiza wananchi kuacha kufanya matukio mbalimbali ya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo pamoja matukio ya mauaji.
Akitolea ufafanuzi wa suala hilo, Mkuu wa Gereza la Isupilo, Mrakibu wa Magereza, Daniel Kayuni amesema kuwa asilimia kubwa moto huo umekuwa ukianzisha na watu ambao hawana ufahamu na masuala ya udhibiti wa moto jambo ambalo limekuwa likileta madhara kwenye maeneo yao.
"Mfano moto wa juzi kuna mwananchi alikuwa anachoma mkaa ndio ambaye amesababisha moto huo ukasambaa mpaka kwenye maeneo yenu ambapo hata sisi tumeingia hasara ya hekari 40 za miti zimeungua kwa moto hivyo hasara ambayo wananchi wanaipata hata sisi tunaipata ," amesem.
Kayundi amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita zaidi ya hekari 400 za miti zimeungua na moto ambapo mpaka sasa bado hawajarudishia upandaji wa miti hiyo.
Ameongeza kuwa ili kukabiliana na suala hilo wanahitaji ushirikiano wa wananchi wa vijiji vinavyopakana na gereza hilo kuweza kuwasaidia kuwabaini watu ambao wamekuwa wakisababisha majanga hayo kwenye maeneo hayo.