Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Moshi awapa siku 7 wanaodaiwa kula fedha za vijiji

Mkuu Wa Wilaya Ya Moshi, Kisare Makori Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori

Sat, 18 Feb 2023 Chanzo: Mwananchi

Mkuu wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Kisare Makori ametoa siku saba kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Kastory Msigala kuwasilisha ofisini kwake taarifa ya watendaji 40 wa vijiji wanaodaiwa kula fedha za mapato ya vijiji.

Makori ametoa agizo hilo leo Februari 18 baada ya Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Siril Mushi kutoa taarifa za matumizi mabaya ya fedha, akiwahusisha watendaji 40 wa vijiji.

Katika taarifa ya Mushi, ambayo ameitoa kwenye kikao cha chama hicho kilichoketi kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani, amesema kumekuwa na udhibiti hafifu wa mapato ya Serikali katika ngazi za vijiji na kata.

Aidha Mushi amesema pia lipo tatizo la kutosomwa kwa taarifa za mapato na matumizi katika vijiji, huku watendaji wakighushi mihtasari ya mikutano na kupeleka halmashauri jambo ambalo limepigiwa kelele na wananchi.

“Kuna tatizo kubwa la watendaji wa vijiji kuiba fedha za umma na hawaitishi mikutano ya kusoma taarifa za mapato na matumizi, wananchi wanalalamika huko, hatuoni hatua zikichukuliwa.

“Wanaghushi mihtasari ya mikutano ya vijiji na kupeleka Halmashauri, hili ni tatizo kubwa sana na linaua chama.

“Nilikwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri akakiri hilo ni tatizo kubwa na kwamba kwenye upelelezi waliofanya wamebaini vijiji 40, ina maana CCM haina kura katika vijiji hivyo 40,” amesema.

Amesema kazi ya Kamati ya siasa ya CCM ni kuelekeza, kusimamia, kuhoji na kuchukua hatua na kwamba hawatakubali kuona uzembe unaoendelea kufanywa na watendaji wa vijiji na Kata, ambao unawaumiza wananchi na kukigharimu chama.

Kufuatia taarifa hiyo, DC Makori ametoa siku saba kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, kumpata taarifa ya watendaji hao 40 waliokula fedha za umma na hatua zilizochukuliwa.

"Mkurugenzi naomba ndani ya wiki moja, nipate taarifa ya jinsi fedha hizo zilivyotumika na watu waliozitumia wamechukuliwa hatua gani.

"Taarifa hii imewasilishwa kwenye kikao cha halmashauri kuu ya chama na mimi ndiyo nawajibika kukieleza chama haya matumizi ya fedha za kodi za wananchi yametumikaje kwa ngazi ya wilaya," amesema Makori.

Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya hiyo, Ramadhan Mahanyu amewataka viongozi wa chama ngazi za kata kuanza kutembelea miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na kwa ile yenye dosari kuitolea taarifa ili hatua zichukuliwe.

"Ndugu zangu viongozi wa Kata, ipo miradi inayotekelezwa katika maeneo yenu, niombe muweke utaratibu wa kuitembelea na kuikagua, msisubiri hadi viongozi wa wilaya waje,” amesema.

Chanzo: Mwananchi