Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Moshi awaonya watafunaji fedha za miradi

DC Akerwa DC Mtanda awaonya watakaotafuna fedha za miradi Moshi

Fri, 5 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mkuu wa Wilaya ya Moshi (DC), Said Mtanda ametoa onyo kwa wanaotafuna fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi kuacha ili fedha zinafanya yale yaliyokusudiwa.

Mtanda ametoa onyo hilo wakati akifungua mafunzo kwa wahasibu kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi kuhusu kodi ya zuio yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kilimanjaro.

Amesema ni jukumu la kila moja kufuata sheria za nchi na taasisi zote zinazofanya miradi ya maendeleo kuhakikisha zinazingatia uzuiaji wa kodi ya zuio, kama sheria inavyoelekeza.

"Fedha za miradi ya maendeleo siyo chakula cha kugawana, kwani Serikali inakusanya kodi, ili kutekeleza miradi na Biblia inasema, rushwa huwapofusha macho hao waonao, hivyo niombe tusijiingine kwenye rushwa, tufanye jazi tuliyotumwa na serikali"

Ameongeza kuwa "Sasa niwatake, mhakikishe fedha zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi, zinatumika kama ilivyokusudiwa na miradi inatekelezwa kwa viwango na tutashughulika na wale watakaochezea fedha za miradi ya maendeleo"

Awali akizungumza meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Masawa Masatu amesema ili Serikali iweze kutekeleza miradi ya maendeleo inahitaji wananchi kulipa Kodi kikamilifu na kwamba, wanaendelea kutoa elimu, ili kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi, analipa kwa wakati.

Ofisa elimu na huduma kwa mlipa Kodi TRA mkoani Kilimanjaro, Odupoi Papa amesema lengo la mafunzo hayo ni kuelimisha juu ya kodi ya zuio ambayo kwa mujibu wa sheria, kila wanapofanya malipo, wanapaswa kuzuia kwa viwango, mbalimbali.

"Kodi hii siyo mpya, iko kwa miaka mingi, lakini hamasa kwa taasisi za Serikali na hata binafsi katika kuizuia kodi hii iko chini, hivyo TRA tukaona tuwaite wahasibu wote, ili kuwakumbusha wajibu wao, wa kuhakikisha kodi hii ya zuio inazuiwa na kuiwasilisha kwa mujibu wa sheria"

Nao baadhi ya wahasibu walioshiriki mafunzo hayo, Richard Mbaga na Elisiana Edward, wamesema elimu kuhusiana na kodi hiyo bado inahitajika kwa wahasibu na kwa wasambazaji wa bidhaa mbalimbali, kwa kuwa bado ni changamoto na wasambazaji wengi wanapoambiwa kuna kiwango kinachohitajika kuzuiwa kama kodi, hupabdisha gharama.

Chanzo: mwananchidigital