Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC, Mbunge watunishiana misuli Arusha

Mkuu Wa Wilaya Ya Arusha Mjini, Felician Mtahengerwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini, Felician Mtahengerwa

Sun, 2 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini, Felician Mtahengerwa amezidi kukoleza moto wa vita ya maneno dhidi yake na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo baada ya kurusha vijembe akisema; 'Mwanaume ni mmoja wilayani, hivyo sina muda wa kubishana'.

Pia ameongeza kuwa kauli anazozisema ni mhemko baada ya kuona mkusanyiko wa watu, wala hakuna ajenda maalumu iliyotolewa.

Mtahengerwa ameyasema hayo leo Jumapili, Juni 2, 2024 eneo la Soko Kuu katika shughuli ya ufanyaji usafi ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya mazingira duniani.

Amesema, Arusha mjini inabeba taswira ya nchi kiutalii, hivyo hawezi kuruhusu wamachinga kupanga bidhaa zao chini kama mmoja wa viongozi anavyotaka.

"Arusha ni mji unaobeba taswira ya nchi kwa jambo hili niwaombe wananchi, hakuna siasa hapo, tena mjue kwenye wilaya kuna mwanaume mmoja tu, hakuna wanaume wawili hivyo mnisikilize mimi kiongozi wenu ninachowaambia ndicho kinachofanyika," amesema Mtahengerwa.

Jiji limeshatenga maeneo ya wamachinga kufanyia biashara, akisema kuwa mwaka huu watatenga maeneo zaidi hadi wafanyabiashara wote waenee hivyo habari ya kupanga barabarani wasahau.

"Hii habari ya kupanga barabarani kuanzia Philips hadi Sanawari tena bidhaa za chakula, hili jambo sio sawa, maana hata watalii wanaokuja ili watuachie hela hawawezi kununua bidhaa chini bali wataenda sokoni," amesema Mtahengerwa na kuongeza;

"Kwa hiyo naomba jambo la usafi wa mazingira iwe ni ajenda yetu ya kudumu, tusifuate mkumbo wa mtu ambaye akiona tu mkusanyiko wa watu anatengeneza ajenda tena isiyoeleweka maana anaenda kadri upepo unavyoenda.”

Awali vita ilipoanzia

Awali katika mkutano wa siku sita za moto za Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, Mei 30, 2024, Mtahengerwa alimtuhumu Gambo kuhusika kwenye ukwamishaji wa miradi ya maendeleo kutokana na migogoro baina yake na wataalamu wa halmashauri pamoja na madiwani.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali kuu imetoa zaidi ya Sh7.5 bilioni lakini zilizotumika hadi sasa ni Sh500 milioni sawa na asilimia 6.4 pekee, huku ikiwa umebaki mwezi mmoja kuisha kwa mwaka wa fedha.

“Tumebakiza mwezi mmoja mwaka wa fedha uishe, lakini malumbano, migongano na kutoelewana baina yao imesababisha tuwaadhibu wananchi wetu bure ambao hawana hatia na mbaya zaidi Serikali imeshatoa fedha hizi lakini zinapokuja kwenye matumizi inakuwa ni changamoto,” alisema Mtahengerwa.

Alipopewa nafasi ya kusalimia wananchi, Gambo alimuonya mkuu huyo wa Wilaya dhidi ya tuhuma anazotuma kwake

“Kiongozi mmoja alisema eti, mambo hayaendi kwa sababu ya mgogoro wa Mbunge, baraza la madiwani na wataalamu, sasa najiuliza hapo mimi naingiaje,” alisema Gambo na kuongeza;

“Naomba Mkuu wa Mkoa, mimi sasa hivi nimetulia wasinichokoze, wasinichokonoe, wasinifuatefuate na watimize wajibu wao, maana DC alitakiwa akuambie kwa nini kwake mambo hayaendi, asinisingizie, maana sio mtendaji wa Serikali, bali ni mtumishi wa wananchi,” alisema Gambo.

Alisema kuwa tuhuma hizo zinazorushwa kwake na Mkuu wa Wilaya ni ishara kwamba ameshindwa kuwasimamia wataalamu wake.

“Ndio maana leo Mkuu wa Mkoa unafanya kazi za kwenye wilaya wakati hayo yote inatakiwa yeye ndio afanye kwa hiyo naomba Mkuu wa Wilaya, nakuheshimu sana na najitahidi kumkwepa sana kwenye kazi zake kwa sababu nataka amani na jimbo letu linataka maendeleo kwa hiyo namuomba asinichokonoe kwa sababu sina mpango wa kugombana naye na asinilazimishe kugombana naye,” alisema Gambo.

Mbali na hilo alisema kuwa ufisadi unaotekelezwa na baadhi ya wataalamu, unakwenda kuwagharimu viongozi wa kuchaguliwa kwenye chaguzi zijazo za Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani, hivyo kumtaka Makonda kuendelea kuwakazia spana.

Mbali na hilo Gambo alimuomba, Makonda kukubali maombi ya machinga ya kuruhusu baadhi ya barabara ambazo hazitumiki sana kufungwa baada ya saa 12 jioni wapange bidhaa zao chini.

"Kwa sababu maeneo ya kufanyia biashara ni madogo, kuna baadhi ya barabara hazina matumizi makubwa baada ya saa 12 jioni, hivyo zifungwe na waruhusiwe kupanga vitu vyao wafanye biashara," alisema.

Chanzo: Mwananchi