Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Mbulu awaweka rumande watumishi watano

21845 Mburu+pic TanzaniaWeb

Fri, 12 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbulu. Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amewaweka ndani watumishi wanne wa halmashauri ya wilaya hiyo na mwenyekiti wa bodi ya Shule ya Sekondari Tumati kwa agizo la Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, wakidaiwa kufuja Sh141. 6 milioni za ujenzi.

Waliotiwa rumande ni ofisa elimu sekondari wa halmashauri ya wilaya hiyo, Ludovick Longino, ofisa ugavi wa wilaya, Faustine Safari, fundi sanifu, Mosses Nguvava, mkuu wa shule hiyo, Kilian John na mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Bryson Panga.

Hatua hiyo, imekuja baada ya Serikali kutenga Sh141.6 milioni za ujenzi wa madarasa matatu mapya, bweni moja na matundu sita ya vyoo lakini wao wakakarabati madarasa manne, maktaba, kukamilisha ujenzi wa bweni na kujenga vyoo na mabafu.

Mofuga akizungumza leo Oktoba 10, 2018 baada ya Naibu Waziri Ole Nasha kumpa siku mbili za kuchukua hatua, amesema hawezi kusubiri siku mbili anachukua hatua papo hapo.

"Haiwezekani darasa moja lijengwe kwa kutumia Sh20 milioni na choo kijengwe kwa Sh18 milioni hii hatuwezi kuvumilia, tunawachukulia hatua ili iwe funzo," amesema Mofuga.

Hata hivyo, ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wa wilaya hiyo kufuatilia suala hilo kwa kufanya uchunguzi na kuwafikisha mahakamani.

Pia, amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Hudson Kamoga kumpa taarifa ya mradi mzima wa ujenzi ulivyofanyika kwenye shule hiyo.

Naibu Waziri Ole Nasha amehoji kitendo cha fedha hizo kufujwa baada ya kupata taarifa ya ujenzi wa shule hiyo iliyosomwa na kuwa wamekamilisha ujenzi badala ya kujenga upya.

"Serikali ya awamu ya tano haivumilii kuona ubadhirifu wa fedha unafanyika bila kuchukuliwa hatua stahiki kwa wote waliohusika," amesema Ole Nasha.

Amesema fedha hizo zingeweza kutumika kumalizia majengo hayo na kujenga darasa moja lakini wenyewe wakamaliza fedha hizo kwa kumalizia ujenzi ulioanzishwa.

Awali, mkuu wa shule hiyo Kilian John amesema walipokea Sh141. 6 milioni za ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya madarasa matatu, bweni na choo cha matundu sita.

John amesema shughuli zilizofanyika ni ujenzi wa choo cha wanafunzi, matundu sita, choo cha wanafunzi wa hosteli matundu manne na bafu vyumba vinne, ukamilishaji wa maktaba, ukamilishaji wa madarasa manne na ukamilishaji wa hosteli.

Fundi sanifu, Mosses Nguvava amesema choo hicho kimetumia gharama kubwa kujengwa kwa sababu ya kutumia mfumo wa kisasa pamoja na mabafu.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Panga amesema waliamua kumalizia majengo hayo yaliyoanzishwa na wananchi baada ya kupata fedha hizo kuliko kuanza kujenga majengo mapya.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz