Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Mbeya ashtushwa wanafunzi 16 kutoripoti shule, aagiza wazazi wakamatwe

Dc Mbeya Dc Mbeyaaa.png DC Mbeya ashtushwa wanafunzi 16 kutoripoti shule, aagiza wazazi wakamatwe

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa ameshtushwa na taarifa ya wanafunzi 16 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza shule mpya ya Sekondari ya Nsalala iliyopo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya kutoripoti tangu Januari 8 mwaka huu.

Malisa ameshtushwa na hali hiyo leo Jumatano, Januari 31, 2024 alipofanya ziara ya kujiridhisha maudhurio ya wanafunzi akiwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya.

“Nimefika hapa kwa mambo makubwa mawili, kwanza kukagua miundombinu ya vyumba vya madarasa, madawati na kujua watoto ambao mpaka sasa wameanza masomo,” amesema Malisa.

“Nimeshtushwa kuona kati ya wanafunzi 98 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza, 16 hawajaripoti huku matarajio ilikuwa kupokea asilimia 100.

“Watendaji mpo, hakuna hatua zinazochukuliwa sasa nawaagiza kuanza msako wa kukamata wazazi na kuwachukulia hatua za kisheria sambamba na kujua wanafunzi hao wako wapi?”amesema Malisa.

Pia, amesema ni lazima hatua zichukuliwe kwa kuwa wakuu wa wilaya wamepewa maelekezo na Serikali kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza ifikapo Februari 15 mwaka huu wasakwe ili waendelee na masomo.

“Nimesikia kuna kauli imeelezwa kuwa, wazazi wamewahamishia shule binafsi, hilo siwezi kuliafiki nahitaji taarifa za ukweli na ofisi yangu ipate taarifa haraka iwezekanavyo, huo sio utaratibu wa sera ya elimu kwa wazazi kujifanyia uamuzi,”amesema Malisa.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya amesema ameridhishwa na uboreshwaji wa miundombinu ya vyumba vya madarasa huku akiwataka walimu watoe elimu bora ili kutimiza ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya elimu nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Stephen Katemba amesema watafanyia kazi maelekezo ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Wilaya kwa kuhakikisha wanawafuatilia wanafunzi 16 ambao hawajaripoti Shule.

Katemba amesema awali, Serikali ilitoa Sh62 milioni kwa ajili ya uboreshwaji wa miundombinu ya vyumba vya madarasa katika shule hiyo inayoishia kidato cha tatu.

Ofisa Elimu Wilaya, Aliko Mbuba amesema katika shule hiyo hakuna upungufu wowote wa miundombinu na walimu kwa kuwa wamejitosheleza katika kila idara.

Mkazi wa Nsalala, Salome Joel ameiomba Serikali kuliwekea mkazi suala la kuwawajibisha wazazi kwa kuwa wengi wamewazuia watoto kuendelea na masomo kwa masilai yao binafsi ya kuwatafutia ajira za utotoni na kuwaozesha wakiwa na umri mdogo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live