Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Ludigija ataka taasisi za haki za binadamu kuwafikia wananchi

Dc Pic DC Ludigija ataka taasisi za haki za binadamu kuwafikia wananchi

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Mkuu wa wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija amezitaka taasisi zinazosimamia haki za binadamu, utawala bora, maadili na rushwa kuhakikisha kwamba haki inatendeka na kujenga jamii yenye usawa.

Ludigija ametoa wito huo leo Desemba 5, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la wadau kujadili changamoto za haki za binadamu, utawala bora, maadili na mapambano dhidi ya rushwa.

Ameelekeza wito huo kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na asasi nyingine za kiraia wanazofanya nazo kazi kwa karibu.

Amesema jamii ya Watanzania hususani wilaya yake ya Ilala inakabiliwa na changamoto nyingi kama vile migogoro ya ardhi, migogoro ya mirathi na unyanyasaji wa kijinsia, hivyo amezitaka taasisi hizo kuwafikia wananchi na kuwasaidia.

"Unakuta mtu anaporwa ardhi yake na watu wenye fedha, wanatengeneza document (nyaraka) za kuonyesha umiliki wa ardhi hiyo. Wakienda Mahakamani wanashinda, huyu masikini anapoteza haki yake.

"Tunataka kutengeneza nchi ambayo watu wote wako sawa mbele ya sheria bila kujali kipato chake, dini yake, kabila lake wala rangi yake," amesisitiza Ludigija.

Amezitaka taasisi hizo kuwasaidia watu wasio na uwezo katika kutafuta haki zao kwa kutoa elimu kwa wananchi sambamba na kupaza sauti juu ya masuala mbalimbali ambayo yanahitaji kukemewa.

Kwa upande wake, Ofisa Mfawidhi wa THBUB - Tawi la Dar es Salaam, Shoma Philip amesema lengo la kongamano hilo ni kukuza uelewa na uzingatiaji wa haki za binadamu, maadili na mapambano dhidi ya rushwa.

"Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka 2022 ni 'maadili, haki za binadamu, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la pamoja kati ya serikali, wananchi na wadau wengine'," amesema Shoma.

Chanzo: Mwananchi