Mkuu wa Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi, Goodluck Mlinga amekerwa na kitendo cha wafugaji kutotiwa hatiani, pindi wakifikishwa mahakamani kwa makosa ya kujeruhi watu, kushambulia mwili na mifugo yao kuharibu mazao mashambani.
Mlinga amedai kuwa wafugaji wengi wanafikishwa mahakamani ila hukumu nyingi wanazopatiwa huachiwa huru kwa kuonekana hawana hatia hivyo kusababisha matukio hayo kutomalizika.
Akizungumza kwenye banda la Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, katika maonyesho ya madini na fursa za uwekezaji Lindi yanayoendelea mjini Ruangwa, amesema changamoto hiyo inamkera.
"Yaani ni changamoto kwa kweli mimi siyo mwanasheria ila sijawahi kuona mfugaji amefungwa hata wiki moja, ili hali wanafanya matukio mengi ya ukiukwaji wa sheria," amesema Mlinga.
Hata hivyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa, Mariam Mchomba, amesema hawezi kuwasemea waliotoa hukumu na kulalamikiwa ila sheria ipo wazi mtu asipokubalia na hukumu ya mahakama anakata rufaa kwenye mahakama ya juu yake.
"Siwezi kuwasemea ila mtu akiona hajapata haki kwenye mahakama ya mwanzo anakata rufaa katika mahakama ya juu ikiwemo ngazi ya wilaya na ngazi ya mkoa, kwani kesi ni mchakato ikiwemo ushahidi usiotia shaka," amesema hakimu Mchomba.
Ameiasa jamii kushiriki katika kutoa ushahidi pindi wakitakiwa kufika mahakamani kwani utaratibu wa kesi hasa za jinai unataka ushahidi.
Kwa upande wake mmoja kati ya wafugaji wa eneo hilo James Aloyce amesema wafugaji siyo wakorofi ila mara nyingi wanaonewa na kunyimwa haki zao.