Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mbaraka Batenga, ameamuru kukamatwa na kushikiliwa rumande, Afisa Mtendaji wa Kata ya Ndirigishi aliyefahamika kwa jina la Mekasi, kwa madai kuwa, ndiye chanzo cha migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
"Yuko ndani mpaka leo, nimemshona ndani...ndio kwa sababu ya ujinga wake, kwa sababu ya vitendo vyake anavyofanya huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria,” amesema DC huyo wa Kiteto, na kuongeza;
“Mimi nitashughulika na mwananchi, lakini; pia nitashughulika na kiongozi, tukinyooshana kwa stahili hii, tutakwenda, huwezi kuwa kiongozi halafu unasababisha migogoro. Hapo hapana, haiwezekani, hatutaelewana."
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Twanga, Kata ya Namelock, leo Ijumaa, Septemba 15.2023, DC Batenga amesema, hatomfumbia macho kiongozi atakaye sababisha migogoro ya ardhi wilayani humo.
"Kuna eneo la hifadhi ya Emboley Murtangos, hili eneo sio la kilimo, watu wanataka kulifanya shamba la bibi...Mtendaji wa Kata na Afisa Tarafa, kasimamieni na mkawaondoe waliovamia...waondolewe walioko mle, hivi ninavyozungumza...na taarifa niione ofisini kwangu, mkieleza namna mlivyo shughulika eneo hilo," amesema.
Amesema akikuta mtu anayefanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya Emboley Murtangos, ataanza na aliyewapa jukumu la kuwatoa, kwa sababu mauaji yameanza kutokea, kuna mtu mmoja ameuawa na wengine nane wamejeruhiwa huko.
"Nianze kuwapima wafugaji wenyewe sasa...wale wote waliovamia hifadhi ya Emboley Murtangos nione mmeshughulika nao namna gani, nione kwa kiasi gani wamekamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria, kwa sababu haiwezekani wewe mfugaji ndio mlalamikaji na mvamizi...na ninyi wafugaji msipovamia hayo maeneo yatakuwa salama,” amesema na kuongeza kuwa;
“Ninyi wenyewe ndio wavamizi namba moja na hapa naagiza pia nipate orodha ya wafugaji ambao wamekamatwa na kuchukuliwa hatua...Mtendaji wa Kata...Afisa Tarafa, hili ndio zoezi na kibarua cha kwanza kwenu, sio kuwaondoa tu, wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria."
Katika ukamataji huo, DC Batenga ameonya: “Kumuondoa mtu unamswaga kwani amekuwa ng'ombe? Ukimswaga anarudi tena, hapana, wakamatwe na washitakiwe; hili ndilo la kuanza nalo nione linafanyika na nishuhudie watu wamekamatwa na wamechukuliwa hatua kabla ya mvua ya mwaka huu kuanza kwa shughuli za kilimo.”
"Kuna wafugaji wana maeneo makubwa sana hawayalimi kazi yao ni kukodisha, tuanze na hao hapo hapo, anakuja na malalamiko...Mkuu wa Wilaya amekataa malisho, hapana; umekataa wewe uliyevamia ambaye pia una mifugo” amesema.
Akionyesha kuwa ameamua kulifanyia kazi kwa nguvu kubwa suala hilo la migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, Batenga amesema wote waliovamia maeneo ya Orkitikiti na Engongengare ni wafugaji.
“Kule Orkitikiti waliovamia wote ni wafugaji, Engongengare waliovamia wote ni wafugaji, wafugaji mnapokuwa wavamizi mnataka nini? Ardhi inaongezeka? Nawaambia hakuna ardhi ya malisho zaidi ya hii mnayovamia wenyewe, nasema mpango wa matumizi bora ya ardhi uheshimiwe, sitaki Kiteto ifunguliwe tena mashamba mapya," amesisitiza DC Batenga
Wakizungumza baada ya kauli hiyo Batenga, baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho cha Twanga wamesema tatizo lililopo ni kutochukuliwa hatua viongozi na watu wanaokiuka sheria za ardhi.
"Ni kweli watu wamevamia maeneo ya kilimo na ufugaji na tunapata hasara haswa sisi wanawake kwa sababu watoto wetu ndio wanaopigana na kuuana huko, kila mwaka watu wanauana, wameshindwa kusimamia hili suala, naweza kusema hata wao ni sehemu ya tatizo ndio maana wameshindwa kusimamia,” amesema Sara Yohana Mkazi wa Kijiji cha Twanga, na kuongeza;
“Tunamshukuru sana Mkuu wa Wilaya kueleza ukweli huu kuwa, kwanini waliovamia hifadhi ya Emboley Murtangos hawaondolewi? Hapa wananchi tumemuelewa vizuri sana Mkuu wetu wa wilaya."
Kwa upande wake Ekia Erokoi, ambaye pia ni Mkazi wa Twanga, amesema: “Wafugaji ndio wavamizi namba moja, wako wafugaji wa Subuko, Twanga, Orpirikata na Namekoc, kwa kweli wanafahamika kabisa,” amesema na kuongeza;
“Hawa wamejazana kwenye hifadhi, wanalima na wengine wanakodisha mashamba maekari na maekari na wameshika maeneo makubwa sana wanayafanyia biashara maeneo hayo wana zaidi ya ekari mia mbili mpaka mia tano."