Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Kilosa amwagia sifa Rais Samia

DC Kilosa Amwagia Sifa Rais Samia.jpeg DC Kilosa amwagia sifa Rais Samia

Mon, 17 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro Shaka Hamdu Shaka amempongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za mradi wa barabara ya lami Rudewa- Kilosa na Kilosa - Mikumi.

Shaka ametoa pongezi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea maendeleo ya mradi huo katika eneo linalojengwa daraja la kuingia Kilosa Mjini.

"Mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Dumila-Kilosa- Mikumi sehemu ya Rudewa- Kilosa yenye urefu wa kilometa 24 umefikia asilimia 90 .Mradi huu unatarajiwa kukamilika Julai, 2023 na kazi iliyobakia ni ujenzi wa madaraja matatu, ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umekamilika na kuendelea kutumika,"amesema Shaka.

Akitoa ufafanuzi wa mradi huo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Mussa Kaswahili amesema barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya mkoa huo ambayo inaanzia Dumila hadi Mikumi.

Ameongeza kuwa awali watumiaji wa barabara hiyo walikuwa wanatumia muda mrefu barabarani hadi kufika wakitokea Dumila kwenda Rudewa au Kilosa kutokana na ubovu wa barabara iliyokuwepo.

"Kabla ya ujenzi wa barabara ya Dumila hadi Kilosa, ilikuwa kutoka Dumila hadi Rudewa ilikuwa ni saa tatu lakini kwa sasa ni takribani dakika 40 tu unakuwa umefika,"amesema Mhandisi Kaswahili

Amefafanua mradi wa Rudewa-Kilosa ulibuniwa ili kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa katika kuongeza ushiriki wako kwenye miradi ya ujenzi wa miundombinu.

"Mradi wa Rudewa-Kilosa ulibuniwa ili kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa, katika mradi kuna wakandarasi 7 walioungana na kuunda Umoja Kilosa JV lengo ni kutumia wakandarasi wazawa badala ya kutumia wakandarasi wa kigeni hapo baadaye,"amesisitiza.

Akiwa katika daraja jipya la Kiyegeya wilayani Gairo, Mhandisi Kaswahili emeeleza kuwa, daraja hilo limejengwa kwa viwango na teknolojka ya kisasa na kumaliza kabisa changamoto iliyokuwa ikitokea hapo zamani hususan nyakati za mvua na hata kusababisha daraja la zamani kubomoka na kuathiri shughuli za usafiri na usafirishaji.

Hivyo Serikali iliiingia katika mpango wa dharura na kutenga fedha haraka kwa ajili ili kujenga daraja jipya la Kiyegeya chini ya usimamizi wa Kitengo cha wahandisi washauri wa TANROADS Mkoa wa kwa kushirikiana na makao makuu.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja la kisasa la Kiyegeya Mhandisi Kaswahili amesema,

"Ujenzi wa daraja la Kiyegeya limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.9 ambao mradi wa ujenzi wa daraja hilo ulikamilika Februari 28, 22022 na linatumika kwa asilimia 100 na kuongeza kuwa

"Naishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga na kuleta fedha ili miradi ya kimkakati ikiwemo mradi huu (ujenzi wa daraja la Kiyegea) itekelezwe na kufungua shughuli za uchumi za nchi na kwa mwananchi mmoja mmoja"

Mkoa wa Morogoro una madaraja takriban 2,029 huku mtandao wa barabara ukiwa takriban kilometa 2070. Serikali inaendelea kutenga fedha ili kuhakikisha barabara hizo zinahudumiwa ili kuweza kuhakikisha kwamba zinapitika muda wote na majira yote ya mwaka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Meneja wa mradi RUDEWA-KILOSA kutoka kampuni ya ushauri ya Pidael JV Consulting Engineers Mhandisi Protas Mwasyoke na msimamizi wa mradi upande mkandarasi, Mhandisi Leons Msoka wamesema kwa mwenendo wa kazi za ujenzi zinavyoendelea na kwa kazi ikiyobakia ya ujenzi wa madaraja matatu, kazi hiyo itakamilika Julai mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live