Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Kilombero akataa kurejea Ikulu ndogo baada ya kukarabatiwa

21236 IKULU+PIC TanzaniaWeb

Mon, 8 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ni jambo la kawaida kwa mtu kurejea kwenye nyumba uliyokuwa ukiishi baada ya kuondoka kwa muda ili kupisha ukarabati, lakini si kwa James Ihunyo, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilombero.

Ihunyo, ambaye kama wakuu wengine wa baadhi ya wilaya, alikuwa akiishi Ikulu ndogo ya wilayani Kilombero, amekataa kurejea kwenye makazi hayo yenye hadhi ya urais tangu mwezi Mei baada ya ukarabati kukamilika.

Badala yake, anaishi katika nyumba aliyopangiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero iliyopo eneo la karibu na Shule ya St Francis Morogoro.

Kwa kumpangia, halmashauri hiyo inalazimika kulipa Sh300,000 kila mwezi kwa ajili ya kodi ya pango, kwa mujibu wa habari ambazo Mwananchi imezipata.

DC Ihunyo alilazimika kuhama Ikulu ndogo kwa muda mwishoni mwa mwaka jana kupisha ukarabati mkubwa wa makazi hayo uliofuatiwa na ujio wa Rais John Magufuli ambaye alifikia kwenye nyumba hiyo, takriban miezi mitatu baadaye.

Uamuzi wa mkuu huyo wa wilaya kukataa kurejea Ikulu ndogo hata baada ya kushauriwa na halmashauri, umeibua maswali ya sababu hasa za mteule huyo wa Rais kukataa kuishi katika makazi anayostahili.

Juhudi za Mwananchi kumtaka azungumzie kitendo chake cha kukataa kurejea kwenye makazi hayo hazikuzaa matunda na badala yake mkuu huyo wa wilaya akamuagiza mwandishi wetu amtafute katibu tawala wa mkoa wa Morogoro azungumzie suala hilo.

“Katibu Tawala ndiye atakupa majibu,” alisema Ihunya akikataa kuongeza neno lolote.

Mwananchi imedokezwa kuwa tangu Julai, mkuu huyo ameandikiwa barua na mamlaka ya mkoa ikimtaka arudi katika makazi hayo ya Serikali ambayo yana huduma muhimu anazostahili, lakini hadi jana alikuwa hajarudi.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandali alisema anachofahamu ni kwamba awali kulikuwa na katazo la nyumba hiyo kutumika baada ya ziara ya Rais, lakini baada ya katazo hilo kuondolewa walimwandikia barua Ihunyo kumtaka arejee katika nyumba hiyo iliyomo ndani ya halmashauri yake.

“Nimemuuliza mwenyewe amesema ameamua kuendelea katika nyumba anayokaa sasa na atalipa mwenyewe Sh300,000 kuliko kurudi nyumba ya Serikali,” alisema katibu huyo.

“Kwa hiyo taarifa ya utekelezaji ni kwamba amependelea alipo sasa, atalipa mwenyewe. Jambo likifika hivyo, hapo mimi sina la kufanya tena.”

Gharama ya ukarabati nyumba ya DC hazikuweza kujulikana, lakini inaonekana kufanyika ukarabati mkubwa wa kuipa hadhi ya kutumiwa na kiongozi wa Serikali.

Malipo kodi ya pango yasitishwa

Ofisi ya katibu tawala wa Kilombero imethibitisha kuwapo kwa suala hilo na kwamba imesitisha malipo ya kodi ya pango baada ya Ihunyo kukataa kurejea kwenye nyumba ya Serikali.

“Alianza kuishi nyumba ya kukodi mwezi Januari mwaka huu ikiwa ni miezi mitatu kabla ya kuwasili kwa Rais na sisi tulianza kumlipia mwezi huohuo kabla ya kusitisha malipo hayo mwezi Aprili,” alisema kiongozi mmoja aliyeomba kutotajwa jina.

“Ofisi ya katibu tawala ililipa kodi ya miezi mitatu ambayo ni Sh900,000 ikiwa ni kodi ya kuanzia Januari hadi Aprili. Kuanzia hapo hakuna fedha iliyolipwa na hadi sasa deni limefikia Sh1.8 milioni.”

Julai 27, Tandali alimaundikia barua Ihunyo kumtaka arudi kwenyue nyumba yake.

Mwananchi imedokezwa kuwa tayari ofisi ya katibu tawala ilishatoa taarifa kwa katibu tawala wa mkoa kuhusu uamuzi wa Ihunyo kuishi nyumba ya kupanga badala ya Ikulu ndogo na kuliacha suala hilo mikononi mwake.

Chanzo: mwananchi.co.tz