Mkuu wa wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi Onesmo Busweru, amewataka wananchi wilayani humo kutunza na kulinda vyanzo vya maji ili miradi ya maji inayojengwa iweze kudumu kwa na kuendelea kuwaondolea adha ya upatikanaji wa maji katika maeneo yao.
Busweru ametoa agizo hilo jana,wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Majalila Halmashauri ya wilaya Tanganyika baada ya kukagua mradi wa maji uliotekelezwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa).
Alisema,maji ni rasimali adhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai wengine na haina mbadala wake,hivyo wananchi wanapaswa kuvilinda vyanzo,miradi ya maji,miundombinu na mazingira ili kuepuka kutokea ukame unaoweza kusababisha vyanzo vyanzo vya maji kukauka.
Alisema, mradi wa maji Majalila ni umekuja kwa muda muafaka kwani umeleta suluhu ya changamoto ya huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa eneo hilo ambao kwa muda mrefu hawakuwa na maji uhakika,badala yake walitegemea visima vya asili kupata maji kwa matumizi yao ambayo hayakuwa safi na salama.
Busweru, amewaagiza viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani humo,kuhakikisha wanatumia sheria,taratibu na kanuni zinazosimamia masuala ya maji kama vile kutofanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo.
Amewataka wananchi wa Tanganyika kutunza mazingira,kuacha kukata miti ovyo na kuchoma moto misitu na kulinda miundombinu ya maji kwani serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza na kufikisha huduma ya maji kwa manufaa yao.
Aidha Busweru, ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wawataalam wa Ruwasa ngazi ya wilaya na mkoa wa Katavi kwa kuendelea kutekeleza na kusimamia vizuri miradi ya maji wilayani Tanganyika.
Alisema, mradi huo na miradi mingine iliyotekelezwa imewawezesha wananchi kupata maji safi na salama na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi badala ya kutumia muda wao kwenda kutafuta huduma ya maji mbali na makazi yao.
Mkazi wa kijiji hicho Neema Joseph, ameishukuru serikali kwa kutekeleza na kuwaleta mradi huo kwani umewasaidia kupata huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo yao na hivyo kutoa fursa kwao kutumia muda mwingi kujikita katika shughuli za maendeleo.
Alisema, amelazimika kuingiza maji ndani ya nyumba yao ili kuepuka kero ya kubeba maji kichwani yanayopatikana mbali na makazi na kuwataka wananchi wengine kuvuta maji majumbani ili kuepuka adha ya kukaa kwa muda mrefu kwenye vituo vya kuchotea maji.
Rebeca Ngangu alisema,kabla ya mradi huo kujengwa walikuwa wanatumia maji ya visima vilivyochimbwa na mikono ambayo hayakuwa safi na salama,kwa kuwa hawakuwa na njia mbadala ili kuokoa maisha yao na mifugo.