Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Kali: Andikeni mirathi kabla hamjafariki

Miradhi Piccc Salum Kali

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati migogoro ya mirathi ikizidi kuibuka katika jamii, wazazi wametakiwa kuandika mirathi na wosia kwa warithi wao kabla hawajafariki ili kuepusha migogoro ya umiliki wa mali inayoibuka wanapofariki bila kufanya hivyo.

Wito huo umetolewa leo Disemba 5, 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima katika maadhimisho ya Siku ya Wiki ya Msaada wa Kisheria na Kujitolea Duniani iliyoadhimishwa kimkoa katika viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza.

Kali amesema kuandika mirathi na wosia kabla haujafa siyo uchuro badala yake unatengeneza mazingira mazuri kwa mrithi na kuepusha migogoro inayoweza kuibuka.

Pia, amewataka wananchi kujengewa uelewa wa kisheria ili kuwawezesha kujieleza na kupata haki yao wanapofika mbele ya vyombo vya kutolea haki kwenye mashauri mbalimbali ikiwemo ya ndoa, biashara na umiliki wa ardhi.

"Watu wasikariri kuwa kuandika mirathi ni uchuro, unapoandika mirathi inakusaidia kuweka mambo yako sawa unapopata changamoto.

“Hii tunaomba watu wa Shirika la Kivulini wafike huko vijijini waelishe jamii umuhimu wa kuandika mirathi," amesema Kali

Suala hilo limeungwa mkono na Shehe wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke aliyesema ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko na migogoro (bila kutaja idadi) ya familia inayohusiana na mirathi hivyo kusisitiza kuwa elimu ya uandishi wa mirathi kwa Umma inahitajika.

"Tumekuwa tukitumia hekima kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo suala la mirathi, ndugu kuwania mashamba, biashara na ardhi, niwaombe ndugu zangu, wazazi na walezi tuandike mirathi kabla hatujafariki," amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la Kivulini, Yassin Ally ameahidi kutanua wigo wa utoaji wa elimu ya kisheria na umuhimu wa kuandika wosia kwa jamii hasa ya vijijini.

Ameongeza; "Tumechapisha majarida na tunayagawa kwa jamii bila malipo kwa lengo la kuongeza uelewa wa kuandika mirathi na wosia ili kujiepusha na migogoro ya kuwania mali wamiliki wake wanapofariki."

Noella John, mkazi wa Mwanza amesema kuandika wosia wa mirathi hakuna tatizo lolote kimila bali inaendekezwa na watu kuwa ni kujitabiria mambo mabaya huku akisisitiza kuwa hatua hiyo inasaidia kuondoa usumbufu mwenye mali anapofariki.

"Kuandika mirathi siyo tatizo na hakuna ubaya ni sisi tu tunaendekeza vitu, unapoandika wosia unaondoa usumbufu na mifano ipo ya watu waliofanya hivyo na kunusuru migogoro kwenye familia zao," amesema

Kupitia maashimisho hayo yaliyoshuhudiwa na Mratibu wa United Nations Volunteers Tanzania (UNV), Christian Mwamanga wakazi wa mkoa wa Mwanza wamepewa elimu ya umuhimu wa kuandika mirathi, wosia, kujitolea na kutambua haki zao.

Chanzo: Mwananchi