Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Jokate awashukia wazazi Kisarawe

11507 JOKATE+PIC TanzaniaWeb

Mon, 13 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo amesema atawachukulia hatua wazazi na walezi watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao shule bila sababu za msingi.

Ametoa kauli hiyo jana Agosti 11, 2018 alipofanya ziara katika Shule ya Msingi Chazige A na B wilayani humo.

Katika ziara hiyo Jokate alikutana na wazee wa wilaya hiyo ili kusikiliza kero zao mbalimbali, kubainisha kuwa wazazi na walezi wasiowapeleka watoto shule watachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Amesema lengo ni kuona vijana katika wilaya hiyo wanapata elimu stahiki kwa faida ya Taifa na wilaya, kubainisha kuwa elimu si ya mwalimu au mkuu wa wilaya, huanzia nyumbani kwa wazazi na walezi.

“Sitawavumilia wazazi au walezi wataoshindwa kuwapeleka watoto wao shuleni. Nitawachukulia hatua kali. Serikali lazima itumie nguvu kwa kuwa Kisarawe ni eneo la viwanda tunataka wasome ili fursa zitakapotokea wachukuliwe haraka,” amesema.

Amebainisha kuwa wataendelea na kampeni ya Tokomeza ziro ikiwa ni  kukusanya fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu pamoja na miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa na vyoo.

Ofisa elimu msingi wilaya ya Kisarawe, Shomari Bane amesema tangu kampeni ya kuondoa ziro imeanza wanawatumia wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni.

"Kwakweli imetusaidia sana maana wanafunzi kuanzia mwaka jana ufaulu wa darasa la saba umeongezeka, tunaendelea kuwahamasisha wazazi wawe na moyo wa kutoa ili watoto wao waweze kufanya vizuri katika wilaya yetu," amesema Bane.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz