Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Jokate atangaza vita wanaowaficha wanafunzi wajawazito

34944 Jokate+pic DC Jokate Mwegelo

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kisarawe. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amesema katika uongozi wake hatawavumilia watendaji na wazazi wanaowaficha wanafunzi wanaopewa ujauzito na kusababisha wahusika kuendelea kuwa huru kwa kukosekana ushahidi.

 

Jokate amesema watakaobainika kufanya mchezo huo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao bila kujali mamlaka na vyeo walivyo navyo ndani ya chama na Serikali.

 

Mkuu huyo wa wilaya aliyasema hayo jana Ijumaa Januari 4, 2019 wakati wa akipokea msaada wa magodoro 20 na matenki mawili ya maji yaliyotolewa na wabunge wa viti maalumu wa Mkoa wa Pwani; Subira Mgalu na Zainab Vullu kwa ajili ya Shule ya Sekondari Maneromango.

 

Kauli hiyo ya Jokate imekuja kufuatia kile alichodai suala la mimba kwa wanafunzi ni changamoto inayoendelea kuitesa wilaya hiyo.

 

Alisema kwa kiasi kikubwa hali hiyo inachangiwa na wazazi na watendaji wa vijiji pamoja na kata kutotoa ushirikiano ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika na badala yake wanashiriki kupoteza ushahidi.

 

“Tatizo kubwa lipo kwa watendaji na wazazi, sasa nawaambia tumekaa na viongozi wenzangu wa wilaya tumesema hatuko tayari tena kuvumilia suala hili,” alisema.

 

Alisema hatua kali zitachukuliwa kwa mtendaji au kiongozi wa kijiji ambaye atashindwa kutoa ushirikiano kufanikisha kesi ya mwanafunzi aliyepewa mimba kuamuriwa kisheria.

 

Kuhusu msaada huo kutoka kwa wabunge, Jokate alieleza kuwa unakwenda kusaidia katika harakati za kuinua kiwango cha elimu wilayani humo na kutokomeza daraja sifuri.

 

Kwa upande wake, Mgalu ambaye pia ni naibu waziri wa Nishati alielezea kuguswa kwake na kampeni ya Tokomeza Zero inayoratibiwa na Jokate na kuunga mkono kwa kuisaidia Sekondari ya Maneromango ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira bora.

 

“Jitihada kubwa zinafanyika kuboresha kiwango cha elimu Kisarawe nami binafsi nimeona niunge mkono, lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira yanayofaa na kupata mahitaji yote muhimu,” alisema.

 

Naye Vullu pamoja na magodoro hayo ametoa pia maji kwa ajili ya matumizi ya walimu na wanafunzi wa  shule ya Maneromango.

 

“Kwa kuwa shule ipo jirani na nyumbani kwangu nimewaruhusu walimu na wanafunzi wachote maji bure, tunafahamu mahitaji ya maji ni makubwa kwa taasisi kama shule lakini kutokana na umuhimu wake niko radhi wachote,” alisema



Chanzo: mwananchi.co.tz