Mkuu wa Wilaya ya Hanang' (DC), Janeth Mayanja amewapa saa 24 watu 31 waliodaiwa kuvamia bwawa la Gawlolo Kata ya Dirma na kuligeuza eneo hilo kuwa shamba kuondoka. Watu hao 31 wamevamia bwawa la maji lililopo kijiji cha Gawlolo linalotumika kwa malisho na upatikanaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani na badala yake kuligeuza kuwa shamba.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Januari 16 Mayanja amesema ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara eneo hilo na kukuta hali ya bwawa hilo siyo nzuri.
Mkuu huyo wa wilaya ameagiza wavamizi hao waondoke ndani ya saa 24 na kwa yeyote atakayekaidi polisi wamkamate na kumfikisha mahakamani.
"Halmashauri ya kijiji ndani ya siku saba muwe mmeunda kamati ya uhifadhi katika eneo hili kwa usimamizi wa halmashauri ya wilaya ya Hanang' ili kulinda na kuhifadhi bwawa hili kwa maslahi ya wananchi wa kijiji hiki na vijiji jirani wanaotumia bwana hili," amesema.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Michael Yae amesema uvamizi huo umetokea tangu Januari 9 mwaka huu na hutumia usiku kufanya shughuli zao za kilimo kwa kupeleka matrekta na hadi sasa ekari 400 zimevamiwa kwa kulimwa.
Amesema bwawa la Gawlolo lina ukubwa wa ekari 2,000 ambalo hutumika kunywesha na mifugo katika vijiji vinne katika kata hiyo ambavyo ni Dumbeta, Mureru, Dirma na Gawlolo.