Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Hai naye awasweka mahabusu vigogo wa Kadco

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wakati mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho akiwaweka mahabusu vigogo wawili wa halmashauri, mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya naye amefanya hivyo kwa watendaji kwa vigogo watano waandamizi wa kampuni ya uendeshaji wa Uwanja wa Ndege Kilimanjaro (Kadco).

Juzi, DC Mbogho aliamuru kuwekwa mahabusu kwa saa 24, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga (DED), Zefrin Lubuva na mtendaji wa mji mdogo wa Mwanga, Justice Valentino.

Mbogho alisema amewasilisha kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), tuhuma dhidi ya vigogo hao.

Alipoulizwa jana kuhusu sababu za kuwaweka mahabusu wawili hao, Mbgho alikataa kutaja tuhuma dhidi yao akisema vyombo vya uchunguzi tayari viko kazini.

“Hawako tena kwangu nilishawakabidhi Takukuru na wameshaandika maelezo na wanaendelea nao. Wakati Takukuru wanachunguza jambo sheria inakataza kutaja aina ya uchunguzi,” alisema.

Mkuu wa Takukuru Mkoa Kilimanjaro, Holle Makungu alikiri kufunguliwa jalada la uchunguzi kuhusiana na tuhuma zilizoibuliwa na Mbogho.

“Ni kweli ofisi yetu pale Mwanga wanafuatilia kujua usahihi wa hizo tuhuma zilizoibuliwa na DC. Naona ameamua apeleke Takukuru kwa sababu ndicho chombo cha uchunguzi,” alisema Makungu.

Vigogo wa Kadco

Imeelezwa kwamba Sabaya aliamuru kuwekwa mahabusu kwa vigogo watano wa Kadco inayosimamia uwanja huo wakiwamo wakurugenzi wawili na wasaidizi wao watatu Alhamis iliyopita.

Vigogo waliowekwa mahabusu katika kituo cha Polisi cha Bomang’ombe, Hai ni wa idara ya operesheni, fedha, masoko na ununuzi ambao waliachiwa kwa dhamana siku iliyofuata.

Alipoulizwa sababu za kufanya hivyo, Sabaya alidai kuwa wanahusika na tuhuma mbalimbali za wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Hata hivyo, ofisa mmoja wa Serikali wilayani Hai ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini aliliambia Mwananchi kuwa anavyofahamu, upo uchunguzi unaoendelea Takukuru kuhusiana na masuala ya ununuzi, hivyo kitendo cha DC kuingilia kinaweza kuvuruga uchunguzi huo.

“Tunajiuliza DC amekuwa chombo cha uchunguzi? Kwanza hao watumishi hawako Tamisemi wako chini ya wizara. Kiukweli hapa mkuu wa wilaya amechemka,” alisema ofisa huyo.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Sabaya alisema, “Ni kweli jambo hili linachunguzwa na Takukuru, lakini kuna tuhuma mpya ambazo lazima mimi kama kiongozi wa Serikali nichukue hatua.

“Kuna hili, wameandaa profoma (ankara kifani) ya manunuzi ya vitu vya Sh130 milioni ndani ya siku moja. Wamekaa vikao vya kupitisha siku moja na kulipa siku moja hii haiingii akilini,” alidai Sabaya.

Kwa mujibu wa Sabaya, baada ya kuwahoji walikwenda kumpa nyaraka feki, hivyo asingeweza kuvumilia fedha za umma kuliwa na yeye akiwa kiongozi wa Serikali akae kimya.

“Kuna jingine, kuna nafasi ya kwenda kujifunza masuala ya ukaguzi wa mashine. Ofisa mmoja badala ya kwenda na mtumishi mwenye jukumu hilo alikwenda na mke wake.

“Sasa hili tuache? Haiwezekani najua wana watetezi, lakini nitahakikisha fedha za umma walizopora wanarudisha,” alisisitiza.

Alisema Kadco ni taasisi ya Serikali hivyo haiwezi kuachwa kujifanyia kila jambo kwa kichaka eti wanapaswa kuwajibishwa na wizara husika tu.

Pamoja na utetezi huo wa Sabaya, kitendo hicho kimeibua maswali kama mkuu wa wilaya alikuwa na mamlaka ya kuamuru kuwekwa mahabusu kwa watumishi walioko chini ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na si Tamisemi.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Kadco, Christopher Mukoma alipoulizwa jana juu ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa wasaidizi wake, alisema anafahamu suala hilo lakini akasema hawezi kusema lolote.

Makungu alipoulizwa kuhusu Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro kuwa na taarifa za DC Sabaya kuwaweka mahabusu watumishi hao wa umma alisema ni vyema yeye mwenyewe akaulizwa juu ya jambo hilo.



Chanzo: mwananchi.co.tz