Juni mwaka 2016, Rais John Magufuli alionyesha matumaini makubwa kwa mwandishi wa habari kijana, Godwin Gondwe baada ya kumteua kuongoza wananchi wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Pengine, Rais alivutiwa na Gondwe kutokana na vigezo mbalimbali alivyokuwa navyo, hasa kutokanan na kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Tawi la Dar es Salaam (Tudarco).
Gondwe, mwanahabari aliyewahi kujihusisha na mambo mengi ya sanaa kama muziki, ushereheshaji na matangazo, akaingia ofisini mwishoni mwa Juni 2016 kuanza majukumu yake mapya ya kumwakilisha Rais katika wilaya hiyo.
Katika mahojiano yake na gazeti hili, Gondwe anabainisha mambo aliyofanya ndani ya miaka miwili na miezi tisa na anaipeleka wapi Handeni.
“Kwanza kabisa nilizunguka kata zote 13 za halmashauri ya Handeni kuhakikisha hakuna uhaba wa chakula,” anasema katika mahojiano na Mwananchi.
“Mkoani Tanga kulikuwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, kwa hiyo muhogo ukaonekana ni zao la kuhimili hali hiyo. Mkuu wa mkoa akaagiza kila kaya iwe na ekari moja ya muhogo.
“Wananchi wakasema hawana mbegu, nikaita wadau wote wa maendeleo ofisini kwangu., World vision wakatuletea mbegu za mihogo na tukawagawana bila malipo na wananchi wangu , lengo likiwa kupata chakula cha kutosha vijana waingie kazini. Mwaka 2017/18 tulizalisha tani 1.6 milioni za muhogo mbichi, kati ya hizo, chakula ilikuwa ni asilimia 30 tu, asilimia zilizobaki tukaanza kutafuta soko.”
Mwandishi: Masoko mnapata wapi?
Gondwe: Nchi nne Afrika zimepewa fursa ya kuuza muhogo mkavu China, ikiwamo Tanzania, inahitaji tani milioni kwa mwaka na Handeni tunaweza kupata zaidi ya tani 500,000 ukikausha. Lakini, viwango vyao wanataka ule unyevunyevu wa muhogo uwe chini ya asilimia kumi, hili tumeliona baada ya kupata soko la kimataifa, sasa tumeanzisha kampeni ya kilimo cha kisasa ili kuwa na tija.”
Tumeanzisha shamba la mbegu la mkoa, kila ekari moja ya muhogo itazalisha ekari 20. Hizi ni juhudi zetu Serikali kusaidia vijana walime nini, wazalishe kwa namna gani na wajue soko liko wapi wauze na pia wakaushe kwa sababu soko la kimataifa liko hivyo.
Tumefanikiwa kupata wanunuzi, walishatokea wengi ila kuna kampuni fulani kutoka Vietnam watanunua kilo moja ya muhogo mkavu kwa Sh300, tumewaambia watuongezee bei. Ili kulima kilimo chenye tija na kupata faida, mkuu wa mkoa amezindua kampeni tayari inaitwa Ardhi ya Tanga ni karimu, ongeza tija, kilimo kinalipa.
Mwandishi: Handeni inatambulishwa na nini?
Gondwe: Handeni inatambulishwa na kilimo, kuna mazao manne ya kimkakati. Tumeweka muhogo na alizeti kama mazao ya muda mfupi. Tumeweka korosho na mkonge kama mazao ya muda mrefu. Tumefanya hivyo kwa sababu soko lipo siyo tu ndani hadi Soko la kimataifa.
Tani moja ya mkonge ni dola 1,800, kilo moja ya muhogo ni Sh300, zaidi ya asilimia 50 ya mafuta yanatoka nje kwa hiyo ni fursa kwa kijana wa Handeni kuaga umaskini.
Mwandishi: Kwani Handeni ina fursa ya kilimo pekee?
Gondwe: Hapana, Handeni tuna madini na kuna fursa za mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi linalotokea Uganda hadi Bandari ya Tanga. Kuna kilometa 54 za bomba hilo ndani ya Handeni na moja kati ya kambi nne zitakazojengwa kwa upande wa Tanzania iko Handeni.
Hatua ya uthaminishaji wa fidia inaendelea na tayari tunaandaa wananchi wetu watumie fursa za ajira wakati wa mradi huo.
Tumeshatoa zaidi ya Sh50 milioni kwa uwezeshaji vijana mwaka jana, tunataka wakae pamoja, lazima wajiandae kwenye mradi huo siyo bahati tu. Kwa kijana yeyote anayehitaji kilimo na ufugaji Handeni ni mahali salama kwake na hakuna sababu ya kukimbilia mijini kutafuta maisha kwa sababu fursa nyingi zipo.
Mwandishi: Nguvu kazi yote ni kiasi na je, inafanya yote?
Gondwe: Halmashauri ya Handeni ina takribani wakazi 400,000 na zaidi ya asilimia 60 kati yao wametambuliwa kuwa ni nguvu kazi. Kundi kubwa ni vijana ambao kwa sehemu kubwa hutegemea kilimo.
Hatuna uhaba wa ardhi, sasa kijana akiona kama fursa itamsaidia sana, wakati mwingine ni mapokeo tu kama Ruge (Marehemu Ruge Mutahaba) alivyokuwa akizungumza.
Mwandishi: Sasa mnafanyaje ili kuitumia nguvu kazi hiyo?
Gondwe: Swali zuri sana, tumeanzisha mazao ya muda mrefu na muda mfupi. Kuna zao la muhogo, mkulima analima ndani ya miezi yake sita anavuna, alizeti miezi mitatu hadi minne mkulima anapata fedha yake, lakini kwa mazao ya muda mrefu ni korosho. Mwaka 2016 haikuwa zao kubwa Handeni ila hadi sasa tumeshapanda zaidi miche 250,000 na tunazifuatilia.
Ukiachana na korosho kuna mkonge, mkonge unahitajika sana duniani kwa sasa. Ni zao la muda mrefu. Mwananchi wa Handeni akijua wajibu wake, akatumia fursa zilizopo basi umaskini kwa heri.
Mwandishi: Hali ya kiwango cha elimu sasa iko hatua ipi?
Gondwe: Mpango wa chakula shuleni umepunguza sana kasi ya utoro mashuleni. Na watoto waweze kufaulu vizuri kwa mfano, mwaka 2016, ufaulu wa wanafunzi ulikuwa ni asilimia 62, lakini baada ya kukutana, tukapeana majukumu na kupeana mikataba na wakuu wa idara na maofisa elimu.
Ufaulu ukaongezeka hadi asilimia 75 kwa mwaka 2017, na mwaka jana ufaulu ulikuwa ni asilimia 82, kimkoa katika viwango vya ufaulu, Handeni inashika nafasi ya nne kati ya halmashauri 11.
Pia, mwaka 2016, wastani wa watoto waliokuwa wanaanza na kumaliza darasa la saba Handeni kilikuwa ni asilimia 18 tu, tulipoanzisha programu ya kumwezesha mwanafunzi aendelee na masomo yake, wastani uliongezeka hadi asilimia 51 kwa mwaka 2017.
Kwa mwaka jana tulienda hadi asilimia 70 na tunajipanga kufikia asilimia 90 mwaka huu. Kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, hakukuwa na tatizo sana ila shule ya msingi ilikuwa changamoto sana. Kwa hiyo tumejipanga kuhakikisha watoto wetu kupitia fursa ya elimu bure wanakwenda shule.
Mwandishi: Vipi kuhusu huduma za afya na maji kwa wakazi wa Handeni?
Gondwe: Hakuna jambo lililokuwa linanisikitisha kama huduma za afya, lakini Serikali hii imewekeza fedha nyingi katika sekta hii kuliko sekta nyingine yeyote ile. Kwa mfano, Handeni tumejenga tumeanzisha akiba ya dawa, hakuna mwananchi atakwenda kupata huduma akose dawa pale.
Lakini, tumeendeleza utekelezaji wa sera ya afya inayoagiza mama asitembee zaidi ya kilomita tano kutafuta huduma za afya.