Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Dodoma amewataja matapeli wa viwanja na hatua atakazochukua

2750072fe4efb2aaed30d0eccf8935f2 MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri

Mon, 13 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amesema serikali imejipanga kuondoa matapeli wa viwanja jijini Dodoma ambao wamekuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi wilayani humo.

Akizungumza hivi karibuni katika kata ya Dodoma-Makulu jijini hapa, Shekimweri alisema migogoro mingi ya ardhi katika jiji hilo takribani asilimia 42 ni inayohusu fidia kutokana na upimaji, upangaji na uuzaji viwanja zaidi ya mara moja.

“Matapeli wa viwanja tutahangaika nao na kuwatia nguvuni na hatutawaachia, labda mahakama ndio ikaawachie.”

“Kwa kiasi kikubwa migogoro hiyo inachangiwa na madalali wa viwanja ambao baadhi ya walikuwa watumishi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA),” alisema.

Shekimweri alisema wengine wanaojishughulisha na biashara ya viwanja ni baadhi ya madiwani ambao wamejiingiza katika biashara hiyo kwa kutumia nafasi zao.

Alisema pia wapo viongozi wa mitaaa hasa wenyeviti wa mitaa ambao wamekuwa wakilaumiwa kutokana na biashara hiyo ambayo imezua changamoto kubwa miongoni mwa wananchi.

Mkuu huyo wa wilaya alisema migogoro mingine inachangiwa na baadhi ya watalaamu wa jiji ambao wamechangia migogoro hiyo kwa takribani asilimia 18 kwa kufanya kazi bila weledi na kusababisha mwingiliano wa umiliki wa viwanja.

“Baadhi yao wamekuwa wakijishughulisha na uuzaji viwanja kwa karatasi badala ya kutumia mfumo wa kompyuta na hiyo husababisha wakati mwingine kuuza viwanja mara mbili na kuibua migogoro ya ardhi,” alisema.

Shekimweri alisema changamoto hiyo ya migogoro ya ardhi inakaribia kupata suluhisho baada ya kamati iliyoundwa ikihusisha wizara na mkoa itakapokamilisha mfumo wa kuwakamata wanaojihusisha na utepeli wa viwanja.

Halmashauri hiyo imesajili jumla ya migogoro ya ardhi 2,870 na kati yake, 690 imeshapatiwa ufumbuzi na iliyobaki ipo katika hatua mbalimbali.

Shekimweri alisema ili kuonesha migogoro hiyo ipo wapi, inahitaji mfumo wa kompyuta ambao umechelewa na hivyo kusababisha utatuzi wa migogoro hiyo kuchelewa.

“Mfumo huo ukikamilika waliohusika wawe wamestaafu, au wako wapi watatakiwa kujieleza na sisi hatutawaachia labda mahakama,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz