Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Chongolo awataka wazazi kuwa wazalendo kwa jamii wanayoishi

Wed, 28 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC) jijini Dar es Salaam, Danieli Chongolo amewataka wazazi kuwa wazalendo na kujitoa kushiriki shughuli za maendeleo kwa manufaa yao wenyewe.

Chongolo ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 28,2019 wakati akipokea mabati 160 kutoka kampuni ya  Bill Ndill Enterprises kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Mbezi Ndumbwi.

"Ninachotaka ni kunyanyua na kuibua hisia za uzalendo na kushiriki shughuli mbalimbali kwa manufaa yetu wenyewe," amesema Chongolo

Amesema kutokana na mazingira ya shule hiyo kutoridhisha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wiki moja kabla ya mtihani wa kumaliza darasa la saba atarekebisha vyumba watakavyofanyia na kuwataka wazazi kujitokeza na kuchangia vitu mbalimbali ili kumuunga mkono.

 Ofisa elimu Wilaya ya Kinondoni, Kiduma Mageni amesema kati ya madarasa 100 kwa sasa ujenzi wa madarasa 24 unaendelea ikiwemo madarasa manne katika shule hiyo.

"Kwa sasa tumepokea Sh32 milioni kwaajili ya vyumba vinne vya madarasa, ofisi ya walimu pamoja na vyoo na fedha nyingine tulizopokea kutoka Serikali kuu na Halmashauri zitatumika kuongeza vyumba viwili vya madarasa," amesema Mageni

Pia Soma

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Judith Kilimo amesema wamekuwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa madarasa, uchakavu na uchache wa matundu ya vyoo kutokana na  idadi kubwa ya wanafunzi.

"Kwa sasa tuna wanafunzi 1,667 ambapo wanatumia madarasa 12 na matundu ya vyoo kumi, sita kwa wasichana na manne kwa wavulana" amesema Kilimo

Amesema hata madarasa yaliyopo yamechakaa na yamekuwa yakivuja wakati wa mvua nakupelekea wanafunzi kushindwa kusoma vizuri.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz