Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Mariam Chaurembo amesema kutokana na chumba cha mahabusu kuwa kidogo atageuza chumba kimoja cha darasa kuwa mahabusu na kuwafungia wazazi wote ambao watoto wao hawajaripoti shuleni.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumapili na kuagiza kuwa kesho Januari 23 saa tisa mchana ndio mwisho wa kuripoti shuleni kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari wilayani humo.
Amesema kuwa atapita shule zote na atakusanya majina ya watoto wote waliofika shuleni na majina ya wanafunzi ambao hawajafika shuleni hadi sasa Ili hatua zichukuliwe.
“Kabla ya kuchukua hatua nataka kujua wangapi wamekuja na wangapi hawajaja kuanzia muda huo watakuja kwa lazima mtoto atakuja shule na mzazi ataenda Polisi kama mahabusu ikiwa ndogo tutawahamishia kwenye madarasa.
“Serikali haiwezi kutoa pesa halafu watoto washindwe kwenda shule sasa msipime wingi wa maji nataka muwe vijumbe waambieni wenzenu kuwa hii ni onyo la mwisho tutaanza kuwalazimisha kwenda shule”
Nae Mwenyekiti wa Halamshauri ya Nanyumbu, Benjamini Masimbo amesema kuwa wilaya hiyo imekuwa ikifanya vibaya katika matokeo jambo ambalo hawatakubaliana nalo.
“Sio siri katika mkoa wetu tunapofika kwenye elimu sisi tuko chini katika ufaulu tunakuwa wa mwisho kwa zaidi ya miaka miwili sio jambo zuri na sio jambo la kuchekelea tunayo mikakati ambayo tunataka ionekane kimatokeo tunapenda tubadilike?” amesema Masimbo.