Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Chamwino aagiza uchunguzi tuhuma uuzaji wa ardhi ya kijiji

Ardhi Tuhuma Kuuza.png DC Chamwino aagiza uchunguzi tuhuma uuzaji wa ardhi ya kijiji

Fri, 12 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Janeth Mayanja ameagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi wa tuhuma za kuuza ardhi bila ridhaa ya wanakijiji inayomkabili Mwenyekiti wa Kijiji cha Igandu, George Mkulahuni.

Hatua hiyo ilikuja baada ya baadhi ya wanakijiji hao, kufikisha madai kwa mkuu wa wilaya hiyo, kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa kijijini hapo na Shirika la Reli Tanzania (TRC) uliolenga kutoa elimu juu ya majaribio ya umeme katika reli ya kisasa (SGR).

Hata hivyo, mwenyekiti huyo amesema mwananchi huyo alitakiwa apate Sh300, 000 na eneo jingine wakati Serikali ilipokuwa ikichukua baadhi ya maeneo kwa ajili ya mradi wa reli.

“Kipindi tunahamisha shule, tulionana na watu zaidi ya 15 ambao tuliwalipa pamoja na yeye alipatiwa fedha, lakini tukamwambia aje achukue, lakini hakuja. Kwa hiyo eneo hilo lipo,” amesema.

Akizungumza katika mkutano huo, Monica Kongawadodo amesema kuwa uongozi wa kijiji ulimpokonya shamba lenye ukubwa wa ekari mbili mwaka jana, lakini haukumpa fedha wala ardhi nyingine.

Mwananch mwingine, Richard Mwingwa amesema huu ni mwaka wa tatu hakujawahi kuitishwa mkutano wa wanakijiji kwa ajili ya kusomewa mapato na matumizi ya kijiji hicho.

“Mpaka hapa nilipo ninawadai Sh178, 000 za ulinzi nilikuwa nalinda mashine ya maji ya kijiji, hadi sasa hawanilipi tena wanauza maeneo ya kijiji, wameshauza maeneo yote hakuna hata moja,” amesema.

Amesema hafahamu kwa nini halipwi fedha zake wakati fedha zimepatikana kutokana na mauzo ya ardhi ya kijiji.

Mwenyekiti wa kijiji cha Igandu wilayani Chamwino, George Mkulahuni akijitetea mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja baada ya kutuhumiwa kuuza maeneo bila ridhaa ya wanakijiji.

Akijibu tuhuma hizo, Mkulahuni amesema kuwa hawakufanya mkutano hata mmoja mwaka jana kwa sababu Oktoba mwaka 2022, alifiwa na baba yake, hivyo alikaa baadhi ya miezi bila kufanya kazi.

Amesema miezi minne iliyofuatia alifiwa na mkewe, hivyo alichanganyikiwa na kushindwa kufanya mikutano hiyo.

Akizungumza mkuu huyo wa wilaya, Mayanja amesema “DAS (Katibu Tawala wa Wilaya) naomba umwambie kamanda wa Takukuru aje kujiridhisha hayo mashamba yameuzwa kwa utaratibu gani."

Amesema Takukuru watakwenda kufanya uchunguzi, ili kufahamu kuwa maeneo hayo yameuzwa kwa utaratibu gani na kisha kuchukua hatua stahiki.

“Kwa sababu utaratibu wa uuzwaji wa maeneo hayo yalitakiwa kuanza kwenye Serikali ya kijiji yaende kwenye mikutano mikuu, wananchi mfanye maamuzi. Sasa kama yamefanywa na watu wachache hilo ni kosa la kisheria,” amesema.

Kuhusu madai ya eneo, Janeth amemuagiza ofisa tarafa kuhakikisha kuwa kabla ya Jumatatu Aprili 15, 2024 Monica awe amekabidhiwa kiwanja chake na apelekewe mrejesho.

Pia ametoa rai kwa viongozi wa vijiji kuacha kuchanganya matatizo ya kifamilia na kazi za Serikali ili kuepusha kuharibika kwa shughuli za umma.

Amewaagiza mwenyekiti na ofisa mtendaji wa kijiji (Katibu), kuwa kuanzia sasa mikutano mikuu ya kila robo ifanyike na vikao vya kamati za mipango na fedha vya kila mwezi ianze kufanyika.

Amesema mwenyekiti wa kijiji kuwa na matatizo ya kifamilia hakuzuii mikutano hiyo kutofanyika kwa kuwa viongozi waliopo ndani ya Serikali ya kijiji wanaweza kuongoza vikao.

Aidha, Janeth alimtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kuiweka kata hiyo katika kata ambazo hazina shule za sekondari, ili kuwaepusha watoto kutembea umbali mrefu.

Sheria inasemaje

Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Vijiji ya mwaka 1999, halmashauri ya kijiji imepewa wajibu wa kusimamia ardhi yote ya kijiji.

Katika kutekeleza wajibu wake, halmashauri ya kijiji itabidi kuzingatia ushauri, mamlaka, uwezo, madaraka, haki na wajibu wa taasisi na mamlaka nyingine zilizotambuliwa na sheria kuhusiana na ardhi.

Hata hivyo, katika kuendesha utawala katika ardhi ya kijiji, halmashauri ya kijiji inafanya kazi kama mdhamini kwa niaba ya wanufaika ambao ni wanakijiji.

Kwa maana hiyo chombo chenye madaraka ya mwisho katika usimamizi wa ardhi ya kijiji ni mkutano mkuu wa kijiji na ugawaji wote wa ardhi ya kijiji lazima uthibitishwe na mkutano huo.

Kisheria ugawaji ardhi kwenye vijiji unatakiwa kuamuliwa na mkutano wa wanakijiji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live