Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi, Onesmo Buswelu amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kutosambaratika na badala yake kushikamana ili kuendelea kudumisha upendo,amani pamoja na kufanya kazi halali za maendeleo ili kuliletea Taifa maendeleo yanayoendana na mabadiliko ya tabia nchi.
Ameyasema hayo katika mdahalo wa maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mpanda Ndogo ambapo amesema ni vyema kuheshimu utulivu na amani ambayo inajengwa na Muungano uliopo.
Hata hivyo, amesema kupitia Muungano, maendeleo mengi nchini Tanzania yakiwemo ya kiuchumi, afya, elimu pamoja na uboreshaji miundombinu ya kijamii unaendelea ili kuhakikisha kila mtanzania anaishi maisha bora.
“Hayati baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume waliweka maisha yao nyuma lakini wakaweka maslahi ya watanzania mbele na ndiyo maana leo hii tunawaambia watanzania umuhimu wa kuwa na Muungano na sisi tunaofuata nyuma yao tuna jukumu la kuulinda, kuutunza na kuudumisha,” amesema DC Buswelu.