Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Halima Bulembo amewataka Wavuvi wote wilayani humo kuhakikisha wanakuwa na leseni za uvuvi pindi waendapo baharini kama sheria inavyoelekeza.
Pia ameelekeza wamiliki wote wa vyombo vyote vya uvuvi wahakikishe vyombo vyao vinasajiliwa kabla ya kujihusisha na shughuli za uvuvi kama Sheria zinavyotaka.
Wito huo ameutoa wakati akizungumza na wananchi wa mitaa ya Muhimbili, Mahenge, Puna Center na Kwa-Morris ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara yake ya mtaa kwa mtaa.
Bulembo amesema kuwa leseni za uvuvi Tanzania Bara zinatolewa chini ya Sheria ya Uvuvi Na.22 ya mwaka 2003 na kanuni za uvuvi za mwaka 2009.
Wakati huo huo DC huyo amesema kuwa licha ya uvuvi haramu kudhibitiwa kwa kipindi cha nyuma lakini umeanza tena nakwamba unafanywa na makundi ya wavuvi wa ndani na nje ya kigamboni.
Kutokana na hali hiyo kama wilaya tayari wameweka mikakati ya muda mfupi na mrefu kwaajili ya kupambana na uvuvi huo haramu.
Ametaja mikakati ya muda mfupi ni pamoja na kufanya doria kwenye maeneo yanayoripotiwa kuwepo kwa uvuvi haramu na kuchukua hatua kwa watakao bainika huku ya muda mrefu ikiwa ni kuimalisha vikundi vya kijamii vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi (BMUs).
Kwa mujibu wa Bulembo, BMUS hizi zipo kila mtaa unaogusa bahari na kwamba mkakati huo utahusu uboreshaji wa mipango yao ya usimamizi ili kuishirikisha jamii kikamilifu kwenye suala la usimamizi wa rasilimali za uvuvi.