Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Bukoba aweka mkazo upandaji miti

14b353508b158c63168e85a1d310fb58 Machali ataka ulinzi wa miti isikatwe

Sat, 2 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, kupitia Baraza la Madiwani kuhakikisha wanafanya marekebisho ya sheria ndogondogo za kulinda mazingira, ili kuimarisha ulinzi wa miti iliyopandwa.

Machali ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Charles Mbuge, alitoa kauli hiyo jana katika maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti Duniani kwa Manispaa ya Bukoba.

Alisema kutokana na gharama za kununua miti kuwa kubwa, ulinzi na sheria vinapaswa kuimarishwa na sheria ndogondogo zinapaswa kuboreshwa, ili atakayekamatwa anang’oa au anachezea mti kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Aliwataka wananchi na wadau kuwa walinzi wa miti iliyopandwa na kuilinda, ili baada ya miaka michache mji wa Bukoba uwe kivutio na kufanana na miji mingine duniani.

"Hii miti imenunuliwa kwa gharama kubwa, tunatakiwa kuilinda, mji wetu wa Bukoba unapaswa kupendezeshwa sana na hii miti, kupitia kwa wazawa wa Bukoba ambao ndio wanainunua wangetamani kuona inakua na mji unapendeza,” alisema.

Mradi wa kupanda miti Rafiki ya Mazingira aina ya Royal Palm, ilianzishwa na mzaliwa wa Bukoba anayeishi Texas, Marekani Justine Kimodoi, ambaye kazi yake ni udereva, ambapo baada ya kutembelea miji mbalimbali na kuona hali ya hewa inafanana na Bukoba, lakini akaona imebadilika na kupendeza kwa sababu ya miti hiyo.

Alirekodi video na kutoa wazo la kuhamasisha na kuwaomba wakazi wa Bukoba wanaoishi nje ya mji, kwa kushirikisha wataalamu wa mazingira ofisi ya Manispaa ya Bukoba kupanda miti hiyo, kwa ajili ya kupendezesha mji wa Bukoba.

Wazo hilo limepokelewa na wazawa wa Kagera na wameanza kuchangia miche na gharama za kuipanda.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mradi huo, Thabith Karani, miche inayohitajika barabara zote mji wa Bukoba ni 80,000. Mradi huo unatarajia kukamilika ndani ya miaka minne.

Hivi karibuni Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alizindua kampeni ya kupanda miti kupendezesha mji wa Bukoba na kuwataka kuupendezesha mji wao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live