Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DAWASA yaita wateja kuhakiki taarifa

0f7d201c04d7fd08901441da63450cec DAWASA yaita wateja kuhakiki taarifa

Thu, 21 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imewataka wateja kujitokeza kuhakiki taarifa zao kwa ajili ya kuboresha upokeaji wa taarifa sahihi za mamlaka ikiwemo upokeaji wa bili za maji safi.

Mkurugenzi wa Biashara Dawasa, Ritamary Lwabulinda amesema uhakiki wa taarifa za mteja ni muhimu kwa lengo la kuwezesha mteja kupata taarifa rasmi za huduma za maji, ikiwemo ujumbe wa bili za maji, matengenezo ya miundombinu pindi yanapotokea kwa wakati.

Amesema kuwa Dawasa imekua ikifanya mawasiliano kuhusu taarifa na huduma mbalimbali kwa wateja wake, kupitia njia mbalimbali za kimawasiliano, ikiwemo simu za mikononi, hivyo ni muhimu kwa ofisi kuwa na kanzidata yenye mawasiliano sahihi ya wateja wake, ili kurahisisha mawasiliano.

"Hili ni zoezi endelevu, na nia yetu Dawasa ni kuwakumbusha wateja kuhakiki taarifa zao, ili waendelee kuwa na mawasiliano hai baina ya Dawasa na mteja," amesema.

Amesema kuwa kwa sasa mamlaka imeboresha mfumo wa utendaji, ambapo mteja anapewa nafasi ya kuhakiki bili aliyotumiwa na matumizi yake yanavyoonekana kwenye mita yake, ili aelewe anacholipa na kuondoa uwezekano wa kutokea malalamiko.

Amesema mteja anaweza kutumia njia mbalimbali za kuhakiki taarifa zake, ikiwemo kutumia barua pepe, kwa kutumia namba ya huduma kwa wateja ambayo ni 0800110064 au kwa kutumia namba ya WhatsApp ambayo ni 0735 202121 au kutumia namba za ofisi ya Dawasa zilizo karibu nao.

"Cha muhimu mteja akifanya uhakiki wa taarifa, anatakiwa kuhakikisha anawasilisha namba ya akaunti yake na namba ya simu anayotaka itumike kupokea taarifa hizo," amesisitiza.

Amewahakikishia wateja juu ya usalama wa taarifa zao kwa kueleza kuwa taarifa za mteja zinatunzwa kulingana na kanuni na taratibu za serikali, hivyo wateja wasiwe na wasiwasi kwa kuwa mamlaka inazingatia vigezo vilivyowekwa vya utunzaji wa taarifa za wateja.

Amesema kuwa mamlaka imeweka njia nyingine mbadala kwa mteja kupata bili yake ikiwa ni pamoja na kupakua Application ya malipo ya serikali mtandaoni yaani GePG.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live