Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), imelazimika kuongeza mabasi manne kwa ajili ya kubeba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam kuwahi shuleni na kurejea nyumbani.
Baadhi ya wanafunzi wakijisomea kwenye basi la mwendokasi, lililokuwa likitoka Kimara kwenda Kivukoni jijini Dar es Salaam jana, baada ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kutenga mabasi maalumu ya kubeba wanafunzi pekee nyakati za asubuhi na jioni, ili kuwarahisishia usafiri wa kwenda shule na kurudi nyumbani
DART imesema iliamua kuja na mpango huo kama sehemu ya kuunga mkono sera ya elimu bure, ambayo imesababisha ongezeko kubwa la wanafunzi wa shule za msingi na za sekondari.
Mabasi hayo yanasafirisha wanafunzi hao kuanzia majira ya saa 12 kamili na saa 12.20 asubuhi mawili yakitokea Kimara kwenda Kivukoni na mawili yakitokea Kimara kuelekea Gerezani.
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Wakala, Dk. Philemon Mzee, alisema hayo alipozungumza na gazeti hili kuhusu mkakati huo wa kusaidia wanafunzi na makundi maalum.
Dk. Mzee alisema mabasi hayo hutoa huduma hiyo pia jioni wanafunzi wanaporudi nyumbani kutoka Kivukoni kwenda Kimara kuanzia saa 10:30 na saa 11:00 na kutoka Gerezani kwenda Kimara.
Alisema huduma hiyo imewasaidia wanafunzi wengi kuwahi shuleni na kurudi nyumbani mapema bila usumbufu waliokuwa wakiupata kwenye daladala.
“Tulianza na mabasi mawili, lakini kutokana na mwitikio kuwa mkubwa tumeongeza yawe manne na ni yale marefu yenye mita 18 ambayo yanabeba watu wazima 150,” alisema Dk. Mzee.
Alisema kwa sasa wanafunzi wa shule sita za Kimara, saba za Kivukoni, 14 za Gerezani na saba za Ubungo wananufaika na mabasi hayo.
“Huduma hii imeanza baada ya kufanya utafiti kwa shule zilizoko jirani na huduma yetu ya mabasi yaendayo haraka kwa kuanzia na shule chache za jirani za Muhimbili, Olimpio, Gerezani na Mchikichini.”
Alisema DART pia inatoa kipaumbele kwa makundi maalum ya wazee, wenye ulemavu na wajawazito kwa kuwa wamewawekea mazingira mazuri kuhakikisha wanakuwa wa kwanza kuingia kwenye usafiri huo nyakati zote.
“Hata wakikuta watu wamekaa kwenye viti ndani ya mabasi kwa wale abiria wanaopandia njiani ni sharti kwamba wapishwe wakae na hilo limekuwa likitekelezwa vizuri tu na tunawashukuru abiria wetu ni waelewa,” alisema.
Derrick Mwambe, anayesoma Shule ya Msingi Mtendeni, alisema usafiri huo umekuwa neema kwao kwa kuwa wanafika shuleni kwa wakati na bila usumbufu.
Alisema wanafunzi walikuwa wakinyanyasika kwa kukataliwa kwenye daladala na kuwasababishia kuchelewa kufika shuleni na kurudi nyumbani wakati wa jioni.
“Nimefurahi usafiri huu raha sana, tuko wenyewe ndani ya mabasi hatubanani na hata tukilipa nauli tunarudishiwa chenji kwa urahisi tofauti na kwenye daladala,” alisema.
Arodia John wa Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, alisema usafiri huo umewafanya kufurahia shule kwa kuwa mazingira ya usafiri ni rafiki na hawanyanyasiki kama zamani.
“Tumekuwa tukisukumwa sukumwa tusiingie kwenye mabasi ya daladala na wakati mwingine tunakaa muda mrefu vituoni, lakini kwa utaratibu wa mabasi haya tunapanda wenyewe na kwa utaratibu bila kusukumana,” alisema.
Mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake anasoma Shule ya Msingi Uhuru Wasichana, Farida Kisenga, aliishukuru DART kwa kuamua kuanzisha utaratibu huo ambao unawawezesha wanafunzi kwenda na kurudi shule bila usumbufu.
Alisema utaratibu huo umekuja wakati mwafaka shule zimefunguliwa na idadi ya wanafunzi imeongezeka maradufu kuhitajika usafiri wa kutosha kuwafikisha shule na mkiwarejesha nyumbani nyakati za jioni.
“Huu ni utaratibu mzuri sana kwa kweli DART wanastahili pongezi kwasababu wanapunguzia watoto wetu matatizo, lakini usimamiwe vizuri, ili uwe endelevu isiwe mwanzoni tu hapa halafu watoto wakarudi kule kule kusukumana na watu wa daladala,” alisema mzazi huyo.