Handeni. Wakati Wilaya ya Handeni ikianzisha kampeni ya Binti Shujaa kumaliza tatizo la mimba shuleni, baadhi ya wanafunzi wa kike wamesema umbali mrefu toka nyumbani hadi shuleni na uhaba wa mabweni ni kati ya sababu za utoro na mimba kwenye umri mdogo.
Wasichana hao wamesema hayo leo Jumatatu Mei 27, 2019 wakizungumza baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela kuwakabidhi baiskeli zilizotolewa na shirika la Comfed Tanzania.
Comfed imetoa baiskeli 120 ikiwa ni jitihada za kupamba na tatizo hilo kwa wasichana wanaoishi mbali na shule wakati wa maadhimisho ya wiki ya elimu inayoendeshwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet).
Mwanafunzi wa Sekondari ya Kwenjugo, Hadija Omary amesema kila siku anatembea kilomita 10 kwenda na kurudi shule, umbali ambao umemfanya wakati mwingine kuacha masomo.
"Nilikiwa nachoka sana na ukichoka ndio bodaboda wanakupa lifti wakikupa mara mbili au tatu unajikuta mnazoeana ndio chanzo cha mimba," amesema Hadija.
Awali, Meneja Mradi wa Camfed Tanga, Martine Zakaria amesema wanafunzi wengi huacha masomo kwa sababu ya umbali jambo lililowasukuma kutumia wiki ya elimu kugawa baiskeli.
Pia Soma
- MADAI: DPP awatuhumu wabunge kwa rushwa, Spika ajibu
- Utalii wa utamaduni washika kasi Japan
- Kesi washitakiwa wa meno ya tembo ya Sh1.466 bilioni Juni 11 na 12
- Watoto 20 kuzibuliwa mishipa na kuzibwa matundu ya moyo kwa Cath Lab
"Wakati Serikali inapambana kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kusoma, mashirika nayo yana nafasi kubwa kusaidiana na Serikali kupeleka elimu yetu mbele," amesema Shigela akijaribu kuendesha baiskeli moja iliyotolewa na Camfed.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Zena Said amewataka wasichana kuwekeza kwenye masomo.