Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chuo cha mipango kujengwa kwa bilioni mbili

Chuo cha mipango kujengwa kwa bilioni mbili

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Jumla ya Sh2.1 bilioni zinatarajia kutumika katika ujenzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kinachotarajiwa kujengwa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Akizungumza wakati wa upokeaji hati ya kiwanja cha ukubwa wa ekari 21, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, Kamishna msaidizi wa Bajeti, Pius Mponzi alisema kiasi hicho kinatarajia kutumika kukamilisha ujenzi huo.

Alisema Serikali kwa kutambua thamani ya elimu nchini, tayari fedha hizo zimeshatengwa hivyo ujenzi unapaswa kuanza mara moja ili kufikia malengo.

“Mradi huu unatarajia kugharimu Sh2.1 bilioni, niagize sasa kuanza ujenzi haraka na ninaamini baada ya shughuli kukamilika, wakazi wa Magu itakuwa ni fursa kwenu kuinua uchumi,” alisema Mponzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chuo cha Mipango, Professa Hozen Mayaya alisema kwa sasa ujenzi unaenda kuanza haraka na matarajio yao ifikapo Juni, 2020, chuo kitakuwa tayari kwa matumizi.

“Ujenzi unaanza mara moja na wataalamu wameshafika eneo husika, lakini kwa kuanzia tutajenga kumbi mbili kubwa zenye uwezo wa kubeba jumla ya watu 1,220, darasa, vyoo na ofisi,” alisema Mayaya.

Naye mkuu wa wilaya ya Magu, Dk Philimon Sengati alisema upatikanaji wa eneo hilo haikuwa kazi ya mtu mmoja, bali ushirikiano na wananchi pamoja na aliyekuwa mmiliki, Kampuni ya Nyanza Road Work Ltd.

“Hii ni fursa kubwa kwa Wilaya ya Magu, lakini niendelee kuwapongeza wananchi wa Kisesa kwa ushirikiano mzuri hadi upatikanaji wa eneo hili, haya ni maendeleo yetu sote,” alisema Sengati.

Chanzo: mwananchi.co.tz