Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chuo Kikuu Mzumbe kukarabatiwa, Sh6.5 bilioni zatengwa

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro.  Serikali ya awamu ya tano imetenga Sh6.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe ambayo yatakuwa na uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 1,000.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Novemba 13, 2018 na makamu mkuu wa chuo kikuu hicho, Profesa Lugano Kusiluka wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mahafali ya wanafunzi 3,724 watakaohitimu kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho. 

Profesa Kusiluka amesema mradi huo wa ujenzi wa mabweni utatekelezwa na Suma JKT na kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikiendelea kutatua changamoto za chuo hicho ikiwemo miundombinu. 

Amesema wahitimu wa fani zote watakaohitimu chuoni hapo wanaweza kuajiriwa au kujiajiri popote kwa kuwa wameandaliwa vizuri. 

Amezungumzia maandalizi ya mahafali Profesa Kusiluka amesema Novemba 14 ,2018 kutakuwa na kongamano la kumkumbuka Mwlimu Julius Nyerere ambapo mada itakuwa ni 'Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu mchango wa elimu ya juu katika kuleta maendeleo'. 

Prof. Kusiluka amemtaja mgeni rasmi katika kongamano hilo kuwa ni makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula na watoa mada ni Profesa Raphael Chibunda ambaye ni makamu mkuu wa chuo cha Sokoine cha kilimo Sua na Dk Mortanus Milanzi kutoka Mzumbe. 

Wengine ni Profesa Honest Ngowi kutoka Mzumbe tawi la Dar es Salaam na Ayoub Rioba ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji  Tanzania (TBC).

Amesema Novemba 15 uongozi Mzumbe watakuwa na baraza la msajili ambalo litawahusisha watu mbalimbali waliowahi kusoma chuoni hapo ambapo mgeni rasmi atakuwa Spika mstaafu Anne Makinda ambapo watazunguzia mchango wa chuo hicho katika kuzalisha wataalamu mbalimbali. 

Naye mratibu wa kongamano hilo, Dk Atanas Ngalawa amesema kongamano litawahusisha wadau kutoka Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambao wataandaa machapisho mbalimbali ya Mwalimu Nyererev na kuuza kwa wadau watakaohitimu. 

Dk Ngalawa amesema ili nchi iweze kufikia kwenye uchumi wa kati lazima mchango wa vyuo vikuu utambulike kwani ndio vinavyozalisha na kuandaa wataalamu wa kozi mbalimbali. 

Amesema tangu Mwalimu Nyerere afariki dunia Oktoba 14, 1999 fursa kwa Watanzania kujiunga na elimu ya juu imeendelea kutolewa ambapo Chuo Kikuu Mzumbe kikizalisha wataalamu kwa uwiano sawa. 

Ameongeza idadi ya wahitimu kwa mwaka huu ni 3724 sawa na ongezeko la asilimia 7.1 la wahitimu wa mwaka wa jana ambao walikuwa ni 3458.



Chanzo: mwananchi.co.tz