Wakazi wa Ubungo - Chaibora na Ubungo – Msewe Jijinj Dar es Salaam wamesema matukio ya ukabaji katika daraja la mto unaotenganisha mitaa hiyo yanatishia usalama wa wapitanjia wanaotumia daraja hilo.
Wakazi wa maeneo haya mawili wanaelezea kufurahishwa sana na uwepo wa daraja hilo, lakini kabla ya kujengwa na baada ya kujengwa unaambiwa matukio ya ukabaji darajani hapo siyo jambo la leo au jana, daraja wanalitaka lakini lina pande mbili... ‘Chungu na Tamu'.
“Mimi nimeishi hapa tangu 1992, kabla ya hili daraja kulikuwa na daraja la miti na hapo aliwahi kukutwa mtu amefariki chini ya daraja baada ya kukithiri kwa matukio ya ukabaji hapa. Sasa baada ya kujengewa daraja hili na TARURA kwakweli limetusaidia sana kupita kutoka eneo moja kwenda lingine. Sasa changamoto ni kwamba hapa kuna ukabaji sana watunwananyang'anywa vitu vyao usiku hapa kwasababu ya giza anayetoka huku hamuoni anayetoka kule ng'ambo”- Martin Mbewe, Mkazi wa Ubungo Chaibora.
Uongozi wa Mtaa wa Ubungo Msewe lilipo daraja hilo, unaweka wazi kuwa wanafahamu vitendo vya uharifu vinavyofanyika darajani hapo na kwamba wameshachukua hatua kukabiliana na uharifu huo ingawa umesisitiza wenyeji kutoa taarifa za uharifu ili washirikiane kuumaliza.
“Ni kweli kuna changamoto ya usalama katika eneo lile, tunachokifanya ni kwamba tuna ulinzi shirikishi lakini nadhani peke yake halitoshi kwasababu wananchi wanatakiwa watoe taarifa wanapoona viashiria vya uhalifu au watu ambao hawawaelewi. Tunafikiria kuweka taa lakini hataa hiyo taa inaweza kuibiwa pia kwahiyo kikubwa ni ushirikiano wa wananchi kutoa taarifa za uharifu"- Maria Thomas Mrimba, Kaimu M/kiti Mtaa wa Msewe.